Alipokuwa akitoka Duniani kwenda mbinguni, Kristo aliwaambia wanafunzi kwamba, anaenda kutuandalia makao. Kila watu wanaposoma hiki kifungu kilichoko Yohana.14:1-3, karibu wote uelewa kuwa Yesu anatujengea nyumba za kukaa. Je, hivyo wanavyofikiria ni kweli? Eeee, hicho kifungu kinazungumzia kuhusu nyumba halisi kama zile tujengazo hapa duniani? Tunaposoma kwa makini, tunachokiona kikielezewa kwa biblia sio nyumba hizi wengi wanazodhania. Wapenzi, ikiwa tutayafahamu haya makao anayoyajenga kristo huko mbinguni, inatupasa tuisome biblia kulingana na ule utaratibu alioupeana Mungu, yaani, “ kifungu juu ya kifungu,….hapa kidogo pale kidogo-Isa.28:10-11”. Kwa njia hiyo, tutajiepusha na kosa la kupunguza au kuongezea katika maandiko, maana Mungu asema kuwa, “ chochote afanyacho hudumu hata milele; hakiwezi kuongezewa kitu wala kupunguzwa kitu-Mhubiri.3:14”. Soma pia mithali. 30:6. Basi, hali tukielewa hivyo, tusome Yohana. 14:2, ambapo yesu mwenyewe anasema anaenda kutuandalia makao. Je, tunajua hapo mahali anapoyandaa hayo makao ni wapi? Tusiwe wa haraka kujibu na wala tusitumie akili zetu wenyewe. Tufuate mwongozo wa maandiko, ili Kristo atuambie. Zote tunakubaliana kwamba kristo kweli yuko mbinguni wakati huu. Ikiwa tutaelewa hayo makao anayoyandaa, ni lazima tujue anavyoyaandaa. Basi tujiulize; ni kazi gani hasa ambayo kristo anafanya mbinguni, ambayo ndiyo maandalizi ya hayo makao? Tumsikilize tafadhali. “ Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha ukuu mbinguni-Waeb.8:1”. Hivyo, tunakubaliana kwamba kristo anafanya kazi ya ukuhani, ndio, ni kuhani wetu anayefanyia kazi yake huko mbinguni. Kwa hivyo, ikiwa kunao maandalizi anayofanya, lazima yawe kwa hiyo kazi ya ukuhani, maana ndiyo anayofanya mbinguni sasa hivi. Tunaelewa kwamba kazi ya kuhani, ni kuwapatanisha watu na Mungu wao, kwa njia ya kuwafundisha, maana imeandikwa, “Sheria ya kweli imo kinywani mwake…..kuwageuza wengi hata waache uovu. Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yapasa watu waitafute sheria kinywani mwake-Malaki.2:6-7”. Zote tunaelewa kuwa, Mungu anataka mwanadamu wa kiroho kama yeye, wa kuitawala dunia-Mwa.1:26. Lakini uumbaji wake unachukua hatua tatu kabla aufikie huo ukamilifu( ujumbe wetu uitwao, “Mchakato wa uumbaji wa mwanadamu”, unao maelezo Zaidi). Tunakubaliana pia kwamba huu mwili wa nyama na damu ni hatua ya kwanza ya huo uumbaji, na kwamba, mwanadamu alidanganyika akiwa kwenye hii hatua, na uumbwaji wake ukakomea hapo, huku akitenganishwa na Mungu kwa kukubali uongo-Isa.59:1-2; Matendo.14:16. Baadaye, Mungu alimtuma mjumbe wake iliaje atukumbushe kile Mungu anataka kutufanya, ambacho ndio sababu ya haya maisha ya huu mwili-Waef.3:9-10( soma ujumbe wetu uitwao, “ Kusudi la mwili”, upate kuelewa Zaidi). Basi, kwa wale wanaousikia huu ujumbe wa Mungu ukiletwa kwetu na Yesu(injili) na kuukubali, wao uanza kuishi kulingana na maelekezo yake. Hii inatuleta kwenye jibu la swali letu, yaani; ile kazi Yesu anayofanya mbinguni. Baada ya mwanadamu kukubali uongo, basi, ule ufahamu alioupokea, ukampa namna ya kuishi ulikuwa ni wa shetani, na hivyo akaumbika sura ya Shetani badala ya ile ya Mungu. Hii ndiyo ilikuwa hatua ya pili ya uumbwaji wake, ambapo, kama angelikubali maagizo ya Mungu, Mungu angelianza kuumba akili na tabia zake ndani ya huyo mtu. Lakini kama ilivyo, alidanganyika, na hivyo akaumbikauongo. Basi, kwa wote wale wanaogundua huu uongo, wao wanamrudia muumba wao ili aendelee kuwaumba mahali aliowachia, maana, hakuna mwingine yeyote yule awezaye kumuumba-Zab.127:1. Hapa ndio tunaona kazi ya Kristo ya ukuhani huko mbinguni ikiingilia, “…Mungu akitusihi katika kristo tupatanishwe nayeye-2Wakor.5:20”. Hebu basi tushikanishe tafadhali. Katika 2 wakor.5:1, tunasoma kwamba, “Kwa maana twajua kuwa, nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibika, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni”. Hapa tunapata uthibitisho kwamba, huu mwili tulionao sio mwisho wa uumbaji wa mwanadamu, maana tunaambiwa kuwa ni wa kuharibika. Hata hivyo, tumeahidiwa mwingine usioharibika unaotoka mbinguni, na ambao, wote wanaoukubali ujumbe wa Yesu wanauelewa kiasi cha kuutazamia mwili huo, maana wanasema, “Kwasababu sisi tulio katika maskani hii twaugua tukilemewa; si kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa ili huu upatikanao na mauti umezwe na uzima-2 Wakor.5:4”. Ukweli ni kwamba, wote wanaomwamini Mungu katika kristo Yesu wanaingia katika hatua ya pili ya uumbaji, ambayo ni ya kuumbika akili na tabia za Mungu, yaani, Mungu akitia ufahamu wake katika akili na mioyo yao, maana anasema, “…nitaziandika sheria zangu mioyoni mwao, na katika akili zao nitazitia-Yerem.31:33”. Hii ndiyo kazi Kristo anayofanya huko mbinguni huku akiwatumia wanadamu aliowachagua kuiendeleza hapa duniani maana anatuambia kuhusu kanisa lake, “…ata mwili wa kristo(waaminio) ujengwe; ata na mpaka sisi sote tutakapoufikia…….kuwa mtu mkamilifu…utimilivu wa kristo-Waef.4:12-13”. Akiyathibitisha hayo, Petro anasema kuwa, “Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya roho-1Petro.2:5”. Huu ni uthibitisho kwamba maskani anayoijenga kristo huko mbinguni kama kuhani ni kuumba akili na tabia za maisha ya Mungu ya kiroho ndani ya hii miili ya nyama, ikiwa ni hatua ya pili ya uumbaji wa mwanadamu. Hii kazi uanza tu hapo mtu anapobatizwa, maana yeye “…upokea roho takatifu-Matendo.2:38-9”. Kuanzia hapo, kazi ya “…kuvua utu wa zamani unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zidanganyazo… na kuvaa utu upya, unaoumbika katika sura ya Mungu…. Inaanza-Waef.4:22-24”. Mtu anapopokea roho takatifu, kuumbika huo mwili wa kiroho kunaanza na, “ tunaishika kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika, yeye aliye kichwa, kristo-Waef.4:15; ona 1Petro.2:2 pia. Huku kuumbika mwili wa kiroho unaoandaliwa mbinguni kunafanyika kwa njia gani? Tutakufananisha na mtu anayejenga nguzo ya sementi. Mtu huyo huwa anatengeneza mbao zenye mfano wa ile nguzo anataka kujenga. Baada ya hapo, yeye ukoroga sementi iliyochanganywa na kokoto na kuimwaga ndani ya hiyo shimo iliyo katika hizo ambao alizoziunganisha. Ikisha kauka, yeye uzitoa hizo mbao, na kile kinachobakia huwa ni muundo sawa sawa ni ule ulikuwa wa hizo mbao, lakini wa sementi. Na vivyo hivyo, sisi tunajuwa kwamba, katika huu mwili, Mungu alituumba kwa mfano wake-Mwa.1:27, kumaanisha, ameumbika vile tulivyo- soma Ufu.1:14-15. Kwa hivyo, kwa vile anataka mtu wa kiroho kama yeye, basi huu mwili wa nyama ni mfano wa ule wa kiroho( hizo mbao tulizoona, ambazo ndani yake, sasa anaumba ile nguzo) anaoendelea kujenga ndani ya kila mtu aaminiye mpaka hapo “…..kristo atakapoumbika ndani yetu-Wag.4:19”. Kiasi kile mtu anavyojitoa kujifunza na kutenda kama Mungu, ndivyo Mungu anazidi kujenga ufahamu na tabia zake ndani ya huyo mtu. Kwa njia hiyo, naye huyo mtu uanza kukua kutoka kwenye hii tabia ya uharibifu, huku akiumbika ile tabia ya umilele “……kufananana mfano huo huo, toka utukufu adi utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana aliye roho- 2Wakor.3:18”. Hii ndio kazi kristo kama kuhani wetu mkuu anayofanya katika hekalu la mbinguni, “… mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema la kweli-waeb.8:2-3”. Tukisoma Zaidi, tunaona kweli kwamba, Kristo anafanya kazi ya kutuumba ule mwili wa kiroho maana, “…anatutakasa na kutusafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea kanisa tukufu…….Waef.5:26”. Tukikumbuka mfano wa agano la kale, wakati Kuhani mkuu anapoingia patakatifu pa patakatifu, makutano yote ya waisraeli walikuwa wanasimama nje kuzunguka hilo hema huku wakifunga mpaka wakati kuhani atakapotoka ndani na kuwekelea mikono yake kichwani mwa yule mbuzi wa azazeli aliyekuwa akitumwa jangwani-Mambo ya walawi.16:20-22. Na vivyo hivyo, wote wanaoendelea kuumbwa huu mwili wa kiroho sasa hivi wanakaa kumtazama Yesu kwa njia ya neno lake mpaka siku ile atakapotoka huko hekaluni akirudi duniani. Hii ndiyo sababu anatuagiza “….tuyatafute yaliyo juu mahali aliko sasa(mbinguni) ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Tunayafikiria yaliyo juu sio yaliyo ya huu mwili..mpaka hapo atakapokuja-Wakolo.3:1-3”. Ni yule tu ambaye ataendelea kujifunza kukaa katika neno kwa njia hii ambaye ataumbika awe kama Mungu, maana anasema ni lazima tuwe watakatifu kama yeye-1Petro.1:16; Mat.5:48. Ndio, ijapokuwa tuko hapa duniani katika hii miili, hatuishi maisha ya dunia hii wala ya miili hii, maana Mungu hakutuumba kwa ajili ya hii miili ya nyama bali, alituumba ili ndani yake, atuumbie miili hiyo iliyo kama ule wake. Ukiangalia vizuri katika maandiko yote, hautaona mahali Kristo anafanya kazi yoyote ya ujenzi mwingine isipokuwa huu wa kumuumba mwanadamu, lakini ni yule tu atakayeamua kuishi hayo maisha yanayoelezwa kwa neno lake.Jihadharini na shetani kupitia kwa maanjenti wake ambao wanafundisha kwamba, Mtu ni kama Mungu na kwamba anachongojea ni kwenda mbinguni akaishi kwa hayo manyumba Yesu anayojenga huko. Huu ndio uongo unaowafanya karibu watu wote wasione haja ya kujifundisha kuishi maisha haya anayofundisha katika biblia, na ambayo ndiyo anayoyaumba ndani yetu wakati huu wa maisha ya huu mwili.Huu mwili wa nyama na damu ulijengwa uwe makao ya Mungu, ili akiwa ndani aweze kuendeleza uumbaji wa mwanadamu ata kumkamilisha-1 Wakor.3:9,17, maana saa hii, “tu kazi yake-Waef,2:10”, “mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate kufanana sawasawa naye-Wakolo.3:10”. Basi, kwa vile anachofanya Yesu Kristo wakati huu ni kuendeleza uumbaji wa mwanadamu ata mwishowe apate mtu aliye kama yeye, yaani wa kiroho-Mwa.1:26”, inabidi kila mmoja wetu kuyatumia haya maisha kwa kujifunza kuishi kama Mungu asemavyo katika neno lake, maana huu ndio utakatifu ambao bila huo, hakuna atakayemwona-Waeb.12:14. Ijapokuwa hatuelezwi kikamilifu vile huu ubadilishaji wa hii miili utakavyokuwa, tunajua wasi kuwa, kwa wale wakati huu wataumbika hii hatua ya pili kikamilifu, yaani, akili na tabia ya Mungu, hapo atakapokuja Yesu, “..ataubadilisha huu mwili wa unyonge upate kufanana na ule wake wa utukufu-Wafilip.3:21”. Kwa hivyo, ijapokuwa anaonekana akiijengea hii miili kule mbinguni, ukweli ni kwamba, anaijenga ndani yetu kama vile tumeona mfano wa mbao. Hii ni kwasababu, hapo atakapokuja, tunaona, “…kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho….wafu wakifufuliwa wasiwe na kuharibika, na walio hai wakibadilishwa na kuvaa kutokuharibika-1Wakor.15:52-53”. Maisha ya Kristo wakati alikuwa hapa duniani ndio mfano wa pekee wa zile hatua tutakazopitia katika huu uumbwaji wa mwanadamu, hata tuufikie ukamilivu. Tunaona vile, wakati alikamilika, baada ya kufa, alifufuka akiwa na mwili wa kiroho(ule wa mbinguni). Hii ilifanyika maana alijifunza “…utiivu kupitia kwa matezo aliyoyapata( sawa na yale tunapitia sasa)… mpaka akakamilishwa-Waeb.5:7-8”. Huku kubadilishwa au kufufuliwa tukiwa na miili ya kiroho ndio hatua ya tatu naya mwisho ya uumbaji wa mwanadamu. Baada ya hiyo, Mungu atakuwa amefikia kusudi lake la kumuumba mwanadamu wa kiroho kama yeye, na atampa kuitawala hii dunia milele na milele.Na hapa pia, Yesu atamaliza ile kazi anayoifanya sasa. Hii ndio sababu atatoka huko mbinguni na kuja hapa duniani kama alivyoahidi akisema, “nikisha waandalia makao, nitarudi tena, niwakaribishe kwangu, ili nilipo nanyi muwepo-Yohana14:3”. Wandugu wapenzi, naamini kufikia hapo, ukweli wa makao ya milele anayoandaa Kristo umeeleweka. Kristo anaandaa miili ya kiroho ndani ya hii ya nyama. Najua wengi hawajajua maana ya kumwabudu Mungu katika roho na kweli-Yohana.4:24. Tuelewe basi. Wakati wahekalu la agano la kale, Mungu alikuwa akijionyesha kwa kuhani hapo ndani, halafu kuhani alikuwa akiwaambia watu vile Mungu amesema. Huo mpango ndio unaoendelea katika agano jipya. Tofauti ni kwamba, kuhani anayetuambia vile Mungu anasema, hayuko hapa duniani, bali yuko katika hekalu la mbinguni. Kwa hivyo, tumeunganika naye kwa njia ya roho yake iliyo ndani yetu. Hii ndio maana anasema kwamba, “ alitufufua pamoja na kristo, akatuketisha pamoja naye(mungu) katika ulimwengu wa roho, katika kristo-Waef.2:6”, “ maana wenyeji wetu uko mbinguni….Wafilip.3:20”. Hii ndiyo sababu amri yetu na neno zinatoka “ zayuni na Yerusalemu wa juu-Isa.2:3; Waga.4:26;waeb.12:22”. Hivyo basi, kila mtu atamaniye kuvikwa hii maskani anayoiandaa Kristo, ni lazima aunganike naye kwa njia ya neno lake, huku akiwa mwangalifu, “….kuenenda sawasawa na vile yeye alienenda-1Yohana.2:6; 1 petro.2:21-22”. Ni kwa njia hii ya kutenda neno lake, Kristo anaandaa hiyo maskani ya milele ndani yetu. Kwa vile yeye alielewa vizuri kusudi la haya maisha ya kimwili, wakati alikuwa katika mwili, hakuujali mwili huu wala kujali aibu, bali, “…aliustahimili msalaba na kuidharau aibu( na hivyo akaumbika akili na tabia ya Mungu; ndipo Mungu alimtuza), naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu-Waeb.12:2”. Kwa vile Mungu anataka kutuumbia hiyo miili sasa, ili baada ya kukamilika atupe kuitawala dunia milele, na Kristo amekuja akatuonyesha vile tutaweza kuifikia hiyo goli, basi, inatupasa kuuchukua huo mfano wake, maana Baba wetu anatuambia “tumtazame Yesu mwenye kuanzisha na mwenye kuikamilisha Imani yetu, ambaye kwa ajili ya furaha( ahadi ya mwili usioharibika na utawala wa milele) iliyowekwa mbele yake, aliustahimili msalaba-Waeb.12:2-3; 1 Pwetro.2:21-22”. Ndugu zanguni, ahadi kwa kila atakayefaulu kujikabidhi kwa Kristo ili ajengwe hiyo maskani ya milele, ni lilo hilo ambayo Mungu alimzawadia Kristo, maana, huyu naye, “ atavikwa uzima wa milele na kutokuharibika, na, atapewa kuketi katika kiti cha enzi cha Kristo, kama vile Kristo alipewa kuketi katika kiti chicho hicho na Baba wetu- Warum.2:7; 1Wakor.15:52-54; Ufu.3:21( ujumbe wetu usemao, “Je, wewe ni mukristo”, unao maelezo Zaidi)”. Ni nani basi kati yetu amepewa kuyaelewa haya tunayoambiwa na Bwana wetu Yesu kristo? Ni nani atamaniye kuongozwa na ukweli hata kuifikia hii ahadi? Kama ummoja wao, basi ukweli ndio huu unaousoma hapa. Jikabidhi kwa Kristo naye atakuandalia hayo makao ya milele, na hakika utarithi pamoja naye katika ufalme wa Mungu hapa duniani milele na milele-Dan.2:44;7:27( kwa maeleza ya kina, soma ujumbe uitwao, “Je utakwenda mbinguni?”). Mwenye masikio na asikia vile roho anavyoliambia kanisa. Ni sauti ya Mungu iliyo katika Kristo Yesu ikikujia kupitia kwa mtumishi wake;
KANISA LA MWISHO LA MUNGU.