Siku moja, nilienda kwenye kikao cha majirani ambao sio wa kanisa. Kufika pale, nilikuta watu wa kile, wanaita viwango tofauti vya kimaisha ( soma ujumbe uitwao, “viwanga vya wanadamu”, kwa maelezo Zaidi), wakiwa wameketi kwenye meza moja, huku kila mmoja akihadithia vile ameendelea, na ile mipango ako nayo kwa sasa ya kijiendeleza Zaidi. Maongezi yote yalikuwa ya kila mmoja, kujiinuana hivyo kuwafanya wale ambao hawajakuwa na mapato sawa wakijidharau na kunyenyekea mbele ya wanaojiinua. Sikujua nisimamie upande gani maana sikukubaliana na yeyote ule, waliojiinua kwa waliojidharau. Basi, baada ya kuwasikiliza kwa muda, roho yangu iliugua huku nikiwa na msukumo wa kutaka kusema la kwangu. Niliposhindwa kuvumilia kabisa, niliinuka na kuwauliza swali. Nikawashangaa na kuwauliza.
Je, tunaelewa kwamba sisi zote hapa hatuna tofauti na mayae, kwamba linapoponyoka na kuanguka, halizoeleki, maana linavunjika mara hiyo? Tunaielewa hii mili tulionayo sasa hivi kuwa hali sawa na hilo yae? Punde tu nilipomaliza kuongea, mmoja wa wale wakujiinua akaamka kwa vitisho na kuniuliza; “ wewe ni nani?” Hilo swali lilinipata bila kutarajia na hivyo basi, nilijibu haraka bila kufikiria na kumwambia; “ mimi ni mimi”. Wengine baadhi yao walicheka, huku mwenye swali akinyamaza asiongee Zaidi. Kimya kilitanda kwa muda, na papo hapo, lile swali likanirudia kwa moyo wangu, na kuniuliza tena kimya kimya; “ Eti wewe ni nani?” Basi, katika harakati la kuwaza nikijaribu kujielewa, Mungu alinifunulia kile ambacho kimekuwa huu ujumbe unaousoma hapa. Nimeamua kuuandika ili nipate kuwa na ushirika na wote wapendao kujielewa vyema.
Kwa hivyo, niko hapa sasa nikikuuliza wewe unayeusoma: Wewe ni nani? Mng’ang’ano tunaouona kwa kila mtu kwenye bidii za kujiendeleza kimaisha ni thibitisho tosha kuwa, mwanadamu hajakamilika bado. Kwa wacha Mungu na wasio mcha, wote hawatosheki na kile walicho sasa. Kila mmoja anajibidiisha kuwa kiwango tofauti, iwe ni kwa upande wa nguvu, hekima, utajiri, eee- taja chochote kile na utakuta sisi sote kwenye mbio za kutafuta kuwa zaidi ya vile tulivyo sasa. Ni kwa nini? Kwa nini hatutosheki na kile tulicho?
HATUJAUMBIKA BADO
Ni baada ya hayo mawazo ambapo, Mungu alinifunulia, hiki ambacho naomba tuwe na ushirika katika kumsikiliza muumba wetu akitufundisha. Mungu wetu alianza kwa kuniambia kuwa, njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake. Kujielekeza hatua zake hakumo katika ufahamu wake-Yerem.10:23. Hapo, na kwa kushangaa kiasi, nilianza kuwaza na kujiuliza tena: Ni kwa nini mwanadamu hana ufahamu wa kujielekeza na kujipangia maisha? Ndipo likarudi lile wazo la bidii za kila mmoja za kutaka kuwa tofauti na alivyo sasa. Wapenzi, katika huu mwili wa nyama na damu, bado hatujakuwa kile Mungu anakusudia tuwe.
Hii ni kwasababu, yeye mwenyewe anatuambia kuwa sasa hivi, tuko kwenye hatua ya kwanza ya uumbwaji wetu- 1 Wakor.15:46. Kwa hivyo, ina maana kwamba, hatujui bado kile tulicho, na vile tunapaswa kufanya ili tuweze kukamilika, isipokuwa yeye mwenyewe atuambie. Hii ndio sababu anatuambia kuwa, ijapokuwa tunayo mipango mingi katika akili zetu, ni kusudi lake pekee ambalo litatimia-Mith.19:21. Ni baada ya Mungu kunikumbusha hivi vifungu ambapo niligundua kwamba, nilikuwa makosa kusema kuwa, mimi ni mimi. Yohana aliyaelewa hayo alipoongozwa na roho kusema kwamba, Wandugu, haijabainika wazi bado vile tutakavyokuwa-1 Yohana.3:2.
Paulo naye vile vile akayashuhudia yaya hayo akisema; kwa sasa, tunaona kidogo, kama kwa kioo, mbali wakati ule, tutaona kikamilivu. Kama hivi ndivyo ilivyo basi, tunapaswa kutumia ufahamu gani kujifahamu, na kuelewa tunachopaswa kufanya katika haya maisha ili tuwe tunaishi katika kweli na haki? Kwa vile sasa tumejijua kama viumbe ambao hawajakamilika bado, ambao bado wako kwenye kiwanda wakiumbwa- Yerem.18: 4-6, basi tunapaswa pia kukubali kwamba sisi ni kiwango kile muumbaji wetu ametufikisha, kumaanisha kwamba, ijapokuwa zote tunao goli moja, hatuko sawa kwa sasa. Kwa nini?
SISI NI CHAGUO LETU
Ili Mungu atufanye kuwa alichotaka wakati alituumba, alipanga kwamba, ni lazima kila mmoja apende kuwa hivyo kwa hiari yake, kumaanisha, ni lazima afanye uchaguzi na uamuzi. Eleweni basi ya kwamba, haya maisha ya kimwili ni kipindi cha uchaguzi na uamuzi, ambapo baada ya kufanya hivyo, Mungu anaenda hatua ya pili ya kutuumba( soma ujumbe uitwao, “ kusudi la mwili”). Tunaelewa kuwa, akili zetu hazina uwezo wa kutengeneza ufahamu. Ni lazima zipate ufahamu kutoka nje, na kuuhifadhi. Tunajua pia kuwa, ufahamu uliohifadhiwa ndani ya akili, ndio tunaotumia kuwaza, kutenda na hivyo, kuishi vile tunaishi. Pia tunaelewa kuwa, kunao asili mbili pekee za ufahamu.
Basi hali tukiyajua hayo, ni wazi kwamba, ikiwa tutajijua, ni lazima kila mmoja aelewe asili ya ufahamu anaoutumia kuishi anavyoishi. Inachukuwa aitha roho ya Mungu, au ya Shetani kuingia mioyoni mwetu ili kuzipa akili zetu ufahamu ambao unahifathiwa, na kutumika kama namna ya kuishi. Kwa hivyo, kile tulicho sasa ni hatua katika harakati ya kufanyika kile tumechagua, iwe ni utiivu kutuelekeza kwenye uzima, au, uasi unaotuelekeza kwa mauti-Kumbu kumbu.30:15. Elewa basi kwamba, kile mtu anachochagua uanzisha hatua ya kuiendea goli fulani, ambayo tukiishaifikia, hapo ndipo tutakuwa na haki ya kusema, mimi ni mimi, maana tutakuwa tumeufikia ukamilivu wa chaguo letu.
Na kwa vile sasa hivi, tuko kwenye hiyo harakati ya kuchagua na kuumbika tunachokichagua, hii ndio sababu kila mmoja hatulii alipo, aking’ang’ania kuufikia ukamilivu wa uchaguzi wake. Wandugu, eleweni kwamba kunao goli mbili pekee za kimaisha, zinazotegemea uchaguzi wa mtu, kama vile kunao aina mbili tu za ufahamu ziletao, aina mbili tu za kimaisha ( ujumbe uitwao, “ Wa ulimwengu upi?”. Unao maelezo ya kina). Katika hii hatua ya kwanza, ambayo ni mwili wa mavumbi, muumba wetu anatuambia kuwa, tu- mavumbi, na wenye maisha mafupi ambao kwa wakati fulani, lazima tufe na kurudi mavumbini-Mwa.3:19; Ayubu.14:2-3; 1 Wakor.15:52.
Kwa wale ambao wamechagua haya maisha ya kimwili kuwa goli lao, na hii ni baada ya kukubali uongo kuwa, wao ni wakamilivu( kama Mungu), hao wako kwenye jitihada kali la kukifikia kilele cha haya maisha ambacho ni kuwa tajiri kushinda wote, wenye sifa, na viwango vya juu Zaidi ya wote. Kwa hivyo, wanajitahidi kuwa watukufu, kulingana na utukufu wa maisha yenyewe ambao ni, Magari, manyumba, na mavazi ya kifahari, yang’aayo. Pia wanajaribu kujiburudisha kwenye burudani za kifahari zilizopambwa kuonyesha utukufu ( soma undani wake kwenye ujumbe uitwao, “ Iweni waangalifu”).
Hii yote inafanyika katika ufahamu wa kwamba, wao wamefikia kilele cha uumbwaji, na kinachobaki ni kuthibitisha kule kuwa kama Mungu ( yaani, watukufu). Hila, matendo yao yanathibitsha kudanganyika kwao, maana tunawaona wakiangaika wakijaribu kufikia kiwango fulani. Je, hizi bidii zao sitawafikisha kwenye goli gani, ambapo wataweza kusema kwa haki kuwa, mimi ni mimi? Hebu tafadhali tupate jibu kutoka kwa yeye ambaye peke yake, ndiye ajuaye. Mungu anatujibu akisema; Mkiishi kwa kuufuata mwili, mtakufa- warum.8:12. Hivyo basi, tukisha kufa, tutakuwa mavumbi. Na kwa vile huu mwili ni wa dhambi, basi, zote tunaelewa kwamba goli la wenye dhambi ni, kuteketezwa jehanamu na kuwa majivu-Malaki.4:3.
Ibrahimu alikuwa na huu ufahamu wa wale wataishi katika lengo la huu mwili tu, maana anasema kuwa goli lao ni kuwa, wavumbi, na majivu-Mwa.18:27. Wandugu, hii ndiyo hatima ya wao waishio kuufuata mwili na vilele vyake, wajikuzanyiao utajiri, wasijitajirishe katika Mungu-Luka.12:21; Zab.49:6,13. Hiki ndicho watakacho kamikika kuwa, na kufikia kama goli la maisha yao, Ambacho ndicho watakachokuwa wakweli kusema, “ mimi ni mimi”, yaani, mavumbi na majivu. Kwa sasa, bado wanang’ang’ana maana hawajafikia hapo, hawajakamilika. Hila tu, wamedanganyika kuhusu ile goli watakaoifikia. Na hii yote ni kwa sababu, ile roho walikaribisha kwa mioyo yao, ambayo iliwapa ufahamu wa kile walicho, na kile wanapaswa kufuatilia katika maisha, ni roho ya udanganyifu, ambayo iliwapa, maisha yandanganyayo na kuharibu-waef.4:22.
GOLI LA MUNGU
Wanadamu wote walianza kwa kuingia kwenye huu mtego wa shetani, na kila mmoja wetu amekuwa, na mpaka wa sasa, kwa kiwango kikubwa, bado tunaenenda katika huu uongo. Lakini Mungu alipanga mpango wa awali wa kumnasua mwanadamu kutoka kwa huu uharibifu. Huu mpango uanza ndani ya moyo wa mtu, kwa kubadilisha yule roho aujaao huo moyo. Hii nayo ubadilisha ule ufahamu wa akili yake, na hivyo kumfanya mtu abadilishe ile namna ya kuishi ambayo pia, ubadilishe ile goli anaoiendea. Tangu mwanzo, Mungu alitaka, na mpaka wa sasa, anataka mtu wa kiroho kama yeye mwenyewe ( soma undani katika ujumbe uitwao, “Mchakato wa uumbwaji wa mwanadamu”).
Kwa hivyo, anawaambia wote wamwaminio na kuukubali huu ujumbe; na kama vile nilivyowaumba katika huu mwili, ikiwa ni hatua ya kwanza, na vivyo hivyo, nitawaumba na kuwafanya viumbe wa kiroho-1 wakor.15:49,53. Wapenzi, hiki ndicho wote wamchao Mungu katika kweli wameamini na kukubali. Je, wewe ni mmoja wao? Uchunguze moyo wako kabla hujajibu tafadhali. Huku kufanyika viumbe wa kiroho ndicho kile wacha Mungu wanang’ang’ania kufanyika katika haya maisha ya kimwili ya sasa. Na kama vile wenye kung’ang’ania utukufu wa kimwili watafanyika kuwa mavumbi na majivu kama goli lao, na vivyo hivyo, hao wanaong’ang’ania kufanyika viumbe wa kiroho watafanyika kuwa roho tukufu yenye uzima wa milele-Warum.2:7.
Hii ndio ile goli la badala. Basi je, ni kitu gani hawa wacha Mungu walicho kwa sasa, na ambacho, wanadhamini kwa nguvu zao zote? Jihadharini msije mkawa baadhi ya wale watiao ushauri giza kwa maneno yasio na ufahamu-Ayubu.38:2. Haya nasema kwa sababu wakati Mungu alikuwa akipanga na kuumba, hatukuweko. Kwa hivyo hakuna vile tutajua vile anaendeleza uumbaji wake, isipokuwa atueleze yeye. Hii ndio sababu anatuambia kuwa, mawazo yake sio yale yetu, wala fikira zake sio zile zetu-Isa.55:7-8. Ni rahisi sana kutia ushauri giza, na kupinga kazi ya Mungu ya kutuumba Zaidi, ikiwa tunafikiria kwa kutumia hizi akili za kimwili, na kuanza kuuliza, lini na vipi, kuhusiana na hali zinazotupata katika maisha, vitu ambavyo Mungu peke yake ndiye ajuaye-Matendo.1:7. Isaya anaita hii hali ya kimwili, kupindua mambo juu chini, huku udongo ukimuuliza mvinyanzi kuhusu jinsi anavyouvinyanga-Isa.29:16. Je, tunajua kwamba, sasa hivi ninavyoandika, wengi wetu tunamuuliza Mungu kuhusu anavyotuumba kiroho, huku tukimlalamikia kila wakati?
TUNAUMBWA KUPITIA HALI
Kila swali la kihesabu lina njia lake la kupata jibu la sawa. Wakati wowote mtu akikosa kutumia ile njia iliyowekwa kutafuta jibu la hesabu fulani,yeye ukosea. Wapenzi, hivi ndivyo kila hali inayotupata katika maisha ilivyo. Kila hali ni hesabu fulani, na kila andiko katika vifungu vya biblia ni njia ya kupata jibu la kila hali bila kukosea, maana, kwa neno, tunajichunga tusije tukakosea katika kila hali-Zab.119:9-11; 2 Tim.3:16-17. Yohana akiongezea hayo anasema, ndani ya neno humo uhai, na huo uhai ndio nuru ya mwanadamu-Yohana.1:4. Ndio, kabla Mungu hajaumba, hakukuwa na chochote, wala nje yake hamna uhai mwingineo ule, maana yeye peke yake, ndiye uhai, ambaye ndani yake, vyote vimeumbwa, vilivyo mbinguni na duniani.
Kutoka kwake na ndani yake, vyote vinaishi-Wakolo.1:16; 1 wakor.8:6. Kwa hivyo, ikiwa tutaishi katika kweli, na kuifikia goli hili la kweli, ni lazima tuwe waangalifu, kuhakikisha tunatenda kile maandiko yasemacho. Ikiwa mtu yeyote anataka kujua, basi eleweni kuwa, maandiko ya biblia ndio mwongozo wa Mungu kwa mwanadamu kuhusu vile tunapaswa kuishi-Yohana.6:63. Hali tukiyaelewa hayo basi, wewe ambao umeamua kuishi maisha ya Mungu, wewe ni nani? Ni lazima tujibu kulingana na vile maandiko yanavyosema. Kwa hivyo basi, wewe ni nani? Mungu anatuambia. Wewe ni…….nini? wewe kwa sasa si kitu, ni bure tu- wagal.6:3. Hai! Kwa nini? Maana Mungu bado hajakufanya kile anachotaka uwe. Kwa hivyo kwa sasa, sisi ni viumbe ambao wako kwenye harakati ya kufanywa kuwa kitu.
Tunafananishwa na, mgeni msafiri, mpita njia anayeelekea kwao, ambaye ni lazima ajihadhari sana asiishi kimwili, maana kitamzuia kufanyika roho-1 petro.2:11. Basi, hali tukikumbuka ya kwamba, kila wakati tunapofundishwa jambo mpya, linatuhitaji kubadilika kutoka kwa lingine la awali, basi, kile tulicho sasa ni hali inayopita, maana tuko katika hiyo hali ya kujifunza na kubadilika. Kwa hivyo, kwa sasa, sisi ni ule uchaguzi na uamuzi tunaoufanya katika kila hatua. Kwa hivyo hebu tuelewe na kujua kwamba, kila wakati tunapohusiana na hali yeyote ile, tunakuwa na uamuzi wa kufanya kati ya hizi fahamu mbili. Moja ambayo inahitaji utendaji kulingana na tamaa za mwili, na ambayo haifuatilii ile njia yakusahihisha hesabu ( kuipitia hali kwa njia sawa), na ile nyingine ambayo ni angalifu, kuhakikisha imetumia ile njia sawa(neno), na ambayo ukaa katika kweli-Warumi.7:23.
Kwa vile, katika huu uamuzi wa kuishi kama Mungu, hatujui tulivyo, mbali tunajifunza kwa Mungu kwa kufuata neno lake, na ambayo inatuelezea vile tutakavyokuwa hapo tutakapokamilika, basi hatushikilii hali yetu ya sasa na wala, hatuipiganii; ila, tunashikilia na kupigania kile Mungu anaumba ndani yetu, yaani, uhaki, Imani, upendo, na Amani-2 Tim.2:22; Waeb.12:14, zile tabia tutakazokuwa nazo hapo tutakapokamilika. Hatujui chochote kuhusu sasa, isipokuwa, kule kuwa hai, kwa ajili ya kuumbika Zaidi kwa njia ya kujifunza kwa Mungu, mpaka hapo tutakapokamilishwa. Hii ina maana kwamba, sasa hivi, hatuna chochote cha kushikilia wala kutetea. Tunao kila kitu cha kufuatilia, yaani ile ahadi- uzima wa milele-1 Yohana.2:25, na hapa ndipo, uhai, mioyo, na bidii zetu zipo, mbinguni-Mat.6:20, maana wenyeji wetu uko huko, na kutoka huko, tunamtarajia mwokozi, atakayeubadili mwili wetu wa udhaifu uwe kama ule wake wa utukufu-Wafilip.3:20-21. Maana hatuna mji wa kudumu hapa, mbali tunautazamia ule ujao-Waeb.13:14. Tunaongelelea na kujifunza maisha ya ulimwengu unaokuja, sio huu wa sasa-Waeb.2:5.
Kwa hivyo, kwa kila hali itupatayo, au tunaojikuta ndani yake, hatuogopi, kuhusunika, wala kulalamika. Hii ni kwasababu, katika kila hali, tunayo neno la Mungu ikituambia namna ya kufanya-Isaya.30:21, na pia, kutufunulia sababu ya kuwepo kwa hiyo hali. Neno la Mungu ndiyo kile tulicho kwa sasa, na ndiyo tunaogopa kupoteza. Kwa hivyo, hii neno ndiyo tunayoipigania na kuilinda kwa nguvu zetu zote, isije ikatuponyoka, maana hii ndio kile kitu tunajijua kuwa, kwasababu, ndiyo uhai wetu-Mith.4:22. Ni uongo mkubwa kusema kuwa, sisi ni sisi, kwa sasa, maana mpaka hapo tutakapokamilishwa na kuwa kile Mungu anatarajia kutufanya, ambacho ndicho anaendelea kutuumba kwacho, bado sisi sio sisi.Kumcha Mungu(kutii amri zake, kuishi kwazo) ndio ile njia tunafuata ili tuweze kufanyika kuwa sisi-Mith.1:7; 19:21, na hii itakamilika wakati Kristo atakaporudi, na kutubadilisha, kutupa miili ya kiroho-Wafilip. 3:21.
Kwa namna lilo hilo, ambalo wanaofuata mwili watasema, “ sisi ni sisi”, hapo watakapokuwa mavumbi na majivu, na vivyo hivyo, wanaomcha Mungu watasema, “ sisi ni sisi”, wakati watafanyika kuwa, roho,wakiwa na uzima wa milele-1 wkor.15:53-54. Basi je, sasa hivi, sisi ni nani? Sisi ni yule roho tunachagua akae mioyoni mwetu, ambaye ndiye anatupa ufahamu wa vile tunaishi, kuishi ambako ndiko kunatuelekeza kufikia kile tutakamilia kuwa. Hivyo basi, wewe unajitayarisha kuwa nani? Hicho kinaamuliwa na ule uchaguzi na uamuzi unaoufanya sasa. . Mungu anatushauri kwamba, tuchague uhai na uzima, ili tuweze kuwa kile alitaka wakati alituumba. . Maana ikiwa tutachagua haya maisha ya kimwili ya sasa, hakika tutakufa na kuwa majivu.
Bwana wetu na mwokozi ndiye anayeongea nasi hapa, akiwatakia wote wenye masikio, maisha mema ya milele.