Wengi wetu tunautazama ulimwengu wa leo kwa mshangao! Tunaona shughuli mbali mbali zikifanyika huku zikiitwa maendeleo. Tunashuhudia kuendelea kwa mabadiliko ya mitindo ya maisha. Bila kusahau masuala ya maisha ya kijamii pia. Tabia za watu dhidi ya
wenzao zimebadilika sana. Mambo mengi katika jamii yanakwenda ndivyo sivyo. Kuna kuenea kwa magonjwa mengi sana na hata mengine hayana tiba; matetemeko ya ardhi, ukame, kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya chakula; naam, karibia katika kila nyanja ya maisha
tunashuhudia kuzorota kwa mambo! Kila mmoja anashangaa ni wapi tulipofika, na wengi wanadadisi ama kufikiria kuhusu mwisho wa dunia. Hebu tujiulize kwamba je! ni kweli mwisho umefika? Na kama ndivyo ilivyo; tunajuaje ili tuwe na hakika? Je! upo mwongozo unaoweza kutupatia ufahamu kuhusu jambo hili?
Katika historia yote, wanadamu wamekuwa na wasi wasi daima kuhusu kuja kwa mwisho wa dunia. Watu wamekuwa wakishangaa daima kuhusu kile kitakachotokea katika maisha mwisho wa mambo haya yote. Mfalme mmoja mkubwa wa dunia wa zamani zilizopita
aliyeitwa Nebukadreza pia alikuwa na wasi wasi huu katika kipindi chake. Aliishi akishangaa na kujiuliza maswali kuhusu ufalme wake na kile kitakachotokea baada yake. Siku moja aliota ndoto; na katika ndoto hiyo aliona sanamu kubwa sana ya mtu iliyotengenezwa kwa aina mbali mbali za vitu. Basi alipokuwa akitafakari na kujaribu kutaka kujua maana ya ndoto hiyo; Mungu wa mbinguni ajuaye mambo yote alimtumia mjumbe wake. Naye mjumbe huyo akamwambia; “yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho” Danieli 2:28. Basi kwa vile Mungu habadiliki, na kile asemacho hudumu milele; hebu na tuufuatilie kwa umakini huo ufunuo wake kwa mfalme Nebukadreza wa Babeli ili tuujue ukweli kuhusu dunia na hatima yake.
MWENDELEZO WA FALME
Je! Mungu alikuwa anamfunulia mfalme nini kupitia kwa ndoto hiyo ambayo anasema “ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti?” Danieli 2:45. Alimwambia; “Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii, iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha. Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua
chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba; miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo. Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote” Danieli 2:31-35. Sasa je! haya yote yanahusu nini hasa? Wapendwa; hapa Mungu wa mbinguni alikuwa akimwonesha mfalme Nebukadreza zile falme zitakazoinuka kuanzia kipindi chake mpaka mwisho pindi ambapo yeye Mungu mwenyewe atakapousimamisha Ufalme wake wa milele duniani. Kwa hivyo kwa wale wasioamini katika kuja kwa mwisho wa ulimwengu huu wa sasa na kusimamishwa kwa Ufalme wa mbinguni duniani, hebu na watambue kuwa mwisho unakuja; naye ni Mungu mwenyewe ndiye ayathibitishaye haya. Hebu tulifuatilieni jambo hili kwa makini tafadhalini. Mungu alimwambia mfalme Nebukadreza kwamba ufalme wake wa Babeli ndio ulikuwa kile kichwa cha dhahabu cha ile sanamu {Danieli 2:38}. Katika historia; sote tunafahamu ya kuwa ufalme wa Babeli uliitawala dunia kati ya miaka ya 721 KK hadi 538 KK.
Baada ya ufalme wa Babeli, uliinuka ufalme mwingine wenye nguvu pia unaoashiriwa na kifua na mikono ya fedha katika ile sanamu {Danieli 2:32}. Huu ulikuwa ufalme wa Waamedi na Waajemi chini ya mfalme Dario ulioitawala dunia kati ya miaka ya 537 KK hadi 333 KK.
Baada ya ufalme wa Waamedi na Waajemi, uliinuka ufalme mwingine unaoashiriwa na tumbo na viuno vya shaba {Danieli 2:32}. Huu ulikuwa ufalme wa Wayunani {Ugiriki} chini ya Alekzanda mkuu, ulioitawala dunia kati ya miaka ya 333 KK hadi 33 KK.
Kisha ukafuatiwa na ufalme mwingine wa nne unaoashiriwa na miguu ya chuma na nyayo za nusu chuma na nusu udongo {Danieli 2:33}. Huu ulikuwa ufalme wa Kirumi ulioitawala dunia kati ya miaka ya 31 KK hadi 476 BK; na kuendelea kuanzia hapo kupitia kwa
kuinuka kwa falme ndogo ndogo mpaka pale Hitla na Musolini wa Italia waliposhindwa na majeshi Uingereza na washirika wake {Agiza jarida letu lisemalo “MNYAMA WA UFUNUO” kwa maelezo ya kina zaidi kuhusu mada hii; nasi tutakutumia bure jarida hilo}.
ULIMWENGU WA SASA
Mpaka kufikia mwaka 1945 BK, tumeona kuinuka kwa falme tisa kati ya kumi zilizotabiriwa katika Danieli 7:24. Kuanzia wakati huo mpaka sasa, ufalme wa Rumi umekwenda shimoni. Lakini kwa vile kile asemacho Mungu ni lazima kitimie; basi tunangojea
kufufuka mara moja kwa ufalme wa Kirumi unaoashiriwa na nyayo za nusu chuma na nusu udongo katika ile sanamu ya ndoto ya mfalme Nebukadreza {Danieli 2:33}.
Ikiwa unafuatilia kwa makini mada hii; basi utakubaliana nasi kwamba hivi sasa sisi tunaishi katika sehemu ya mwisho ya sanamu ile; yaani katika nyayo za miguu yake. Sasa je! Si kweli kwamba tunaishi katika siku za mwisho wa ulimwengu huu? Ni kitu gani alichosema
Mungu kupitia kwa Yesu kuwa kitakuwa ishara ya siku za mwisho ambacho sasa tunakishuhudia katika maisha ya kila siku? Katika siku za Nuhu, pindi ambapo gharika ilikaribia kuja kuifunika dunia; “Dunia iliharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma…BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote” Mwanzo 6:11,5.
Akiuzungumzia wakati huu wa sasa, Kristo alisema; “kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu {yaani siku za mwisho}” Mathayo 24:37. Sasa je! Wapendwa; hali haiko hivyo kila mahali katika dunia hii?
Tunashuhudia vitendo vya rushwa zaidi, vurugu sana, maovu zaidi, kizazi cha watu wenye mioyo ipendayo fujo, mauaji, ubakaji na kila aina ya uovu unaoweza kuufikiria unafanyika leo.
Hali hii inautimiza unabii huo wa siku za mwisho kuwa kama siku za Nuhu. Katika kipindi cha Sodoma na Gomora, pindi ambapo miji hiyo ilikaribia kuteketezwa kwa moto; watu walijihusisha na masuala ya ushoga {yaani ngono za jinsia moja} kwa kiasi kikubwa sana, hata wakati malaika walipomtembelea Lutu, watu waliizingira nyumba yake huku wakimwambia, “Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? uwatoe kwetu, tupate kuwajua” Mwanzo 19:4-5.
Akiendelea kuuzungumzia wakati huu wa sasa, Kristo alisema; “kama ilivyokuwa katika siku za Lutu…hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu {katika siku za mwisho}” Luka 17:28-30. Sasa je! hali hii siyo iliyopo sasa kote duniani, watu wakiililia
na kuandamana katika mataifa yote wakidai kuhalalishwa kwa ngono za jinsia moja {ushoga} pamoja na uhuru wa kushiriki vitendo hivyo hadharani?
Wapendwa; kwa uthibitisho huu, tukiujumuisha na historia ya ile sanamu ya ndoto ya mfalme Nebukadreza inayoonesha kuwa imefikia katika nyayo za miguu yake hivi sasa; basi ni ukweli ulio wazi kabisa kwamba sasa ulimwengu umefika mwisho wake! Kulingana na ile
ndoto, pamoja na kutimizwa kwa ishara nyingi zilizotolewa; je! tuko wapi sasa na ni nini tunachosubiri? Wapendwa; tunangojea kufufuka na kuinuka kwa mara ya mwisho kwa ufalme wa Rumi ambao utakuwa ndio zile nyayo za ile sanamu. Ufalme huo wa Rumi unakwenda
kuinuka hivi sasa kwa jina la Umoja wa Ulaya. Baada ya kuinuka kwake na kumchagua mfalme mmoja autawale Umoja huo; basi wakati ukiendelea kutawala, kushikilia na kukandamiza uchumi wa dunia, majeshi na shughuli zote za kijamii; lile jiwe tuliloliona katika ile ndoto
litakuja na kuupiga, na kuvunja-vunja kila kitu cha sanamu hiyo. Maana Mungu wa mbinguni anatuambia kwamba; “Na katika siku za wafalme hao {Umoja wa Ulaya} Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele” Danieli 2:44.
Kwa hivyo basi wapendwa; hii ndiyo Historia ya Dunia, tangu enzi za ufalme wa Babeli mpaka kuja kwa Ufalme wa Mungu hivi karibuni. Basi tambueni kwamba tunapozungumzia mwisho wa ulimwengu huu, ufahamu wetu unatokana na Neno la Mungu wa mbinguni kama
tulivyowaonesheni katika jarida hili, na wala si mawazo na fikira zetu wenyewe {Agiza jarida letu lisemalo “MNYAMA WA UFUNUO” kwa maelezo ya kina zaidi kuhusu habari hizi}. Basi katika namna ile tuliyoiona katika habari za falme zilizotajwa katika ile sanamu ya
ndoto ya mfalme Nebukadreza, zikainuka na kutawala kisha zikapita; fahamuni pia kwamba Ufalme wa Mungu {lile jiwe lililoipiga sanamu na kuivunja-vunja} unakuja hivi punde tu; maana “ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti” Danieli 2:45. Tunangojea sasa kuinuka kwa Umoja wa Ulaya kuitawala dunia, utakaosababisha migogoro mingi duniani. Utawala wa Umoja huo utaishia pale utakapokuwa umeyakusanya majeshi kuizingira Yerusalemu. Basi Mungu wetu anatuambia; “hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia” Luka 21:20. Vita hivi vitakuwa ni kati ya majeshi ya Ulaya dhidi ya majeshi ya Mashariki; yaani muungano wa majeshi ya Urusi, China, Japani na nchi nyingine nyingi za Asia na ukanda wa Kiarabu; zote zikipigania kuutawala mji wa Yerusalemu. Basi wakati huo ndipo atakapokuja Yesu Kristo kama alivyosema; “nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu…hapo ndipo atakapotokea BWANA…Naye BWANA atakuwa Mfalme juu ya nchi {dunia} yote; siku hiyo BWANA atakuwa mmoja, na jina lake moja” Zekaria 14:1-4,9 {Agiza kitabu chetu kisemacho “UFALME WA MBINGUNI” kwa maelezo ya kina zaidi}.
Basi wapendwa; kwa ye yote yule atakaye kufahamu zaidi habari hizi pamoja na kile apaswacho kufanya hivi sasa ili aje kuwa na sehemu katika Ufalme wa Mungu ujao, na awasiliane nasi kwa mafunzo zaidi. Masomo yetu yote yanatolewa bure kabisa pasipo malipo utakayotozwa. Pia tunafundisha ukweli wa Biblia pekee na wala si mafundisho ya kimadhehebu ya kidini wala mapokeo ya wanadamu kama ilivyozoeleka.
Majarida haya yenye mada mbali mbali za masomo ya Biblia yapo tayari kwa ajili yako. Agiza sasa tukutumie bure ili ujifunze zaidi na ufahamu hatima ya maisha yako. Baadhi ya majarida hayo ni pamoja na:
- NI WAPI PA KUANZIA?
- JE! WEWE NI MKRISTO?
- MNYAMA WA UFUNUO,
- KATIKA MILENIA,
- THAMANI YA UKRISTO,
- TAFUTENI HESHIMA,
- KATIKA KUTAFUTA AMANI,
- MITI MIWILI,
- SHETANI NI NANI?,
- KUOKOLEWA KWA NEEMA,
- HUYU NI SHETANI,
- UJUZI WA MAWASILIANO,
- SHERIA ZA KIAFYA n.k.
Vitabu hivi pia vinakungojea wewe;
- UFALME WA MBINGUNI,
- SIKUKUU ZAMUNGU,
- AMRI KUMI,
- KIFO NA KIYAMA,
- MISINGI YA IMANI YA KANISA LA MUNGU,
- DINI ZA MITINDO n.k.
Basi wasiliana nasi kwa anuani zifuatazo;
KANISA LA MUNGU – TANZANIA
Idara ya uandishi na usambazaji – Mwanza
Simu; +255 753 359 179, +255 688 359 179 & +255 655 659 179.
Barua pepe; Ukweliwabiblia@yahoo.com.sg
Idara ya usambazaji;
Arusha – Simu; +255 754 028 574 & +255 782 422 216.
Dar es Salaam – Simu; +255 762 055 056 & +255 672 611 204.
Mara – Simu; +255 755 409 202.
KANISA LA MUNGU – KENYA
Idara ya uandishi na usambazaji – Nairobi
Simu; +254 739 434 639.
Barua pepe; endcog@gmail.com
KANISA LA MUNGU – UGANDA
Idara ya usambazaji – Kampala
Simu; +256 754 167 854.
Neema, rehema na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana wetu Yesu
Kristo ziwe nanyi. Uweza, mamlaka na ufalme ni vyake tangu milele, sasa na hata milele;
Amina.