Tunaishi katika ulimwengu ambao ni wachache sana wanaoufahamu. Muulize mtu ye yote yule kuhusu cho chote kile kihusucho maisha, majibu utakayopata yatakuwa ni ya kubahatisha tu; hayana uthabiti wo wote. Mashirika yetu ya uma yana tamaduni na mila zinazotumika kuongoza watu katika namna ya kuishi na kuhusiana wao kwa wao. Ukiziangalia hizi tamaduni na mila, utakuta kwamba zinafuatiliwa kulingana na matakwa ya walio wengi.
Kwa hivyo, kila mtu hufanya na kuishi kwa kuwatazama wengine kama kioo chake; yaani, mtu hutenda kwa kuzingatia jinsi wengine wasemavyo, wanavyoonelea, na ni kipi kitawapendeza, n.k. Naam, ni mfumo ambao mtazamo wake ni wa kibinadamu. Matokeo ya kuishi hivyo, kujaribu kuishi kulingana na maoni, matakwa na mapenzi ya wengi, kumeleta vurugu na ukosefu wa haki. Katika jitihada za
kutafuta kibali mbele ya wanadamu wenzetu, tumeishi maisha yenye huzuni na mifadhaiko.
Mtu anaweza kuogopa kutenda haki kwa sababu walio wengi hawakubaliani nayo. Anapokataliwa na walio wengi, anaona haya na kujiona duni kwa wengine. Anapokubalika, anafurahia na kujiona kuwa shujaa, na hujigamba huku akiendelea kutafuta kupendwa zaidi na watu. Lakini tukiangalia matokeo ya kupendwa ama kutopendwa, tunaona yakiwa sawa. Anayepuuzwa {asiyependwa} hupigana
kutafuta kukubalika na kuonesha msimamo wake mbele ya wengine. Anayekubalika {anayependwa} naye pia hupigana kujaribu kuwafanya wengine wapuuzwe ili abaki kuwa mwenye kusifiwa peke yake. Ukweli ni kwamba, huu mfumo umeleta vurugu na vita katika ulimwengu wa leo. Pia umewafanya wanadamu kuwa watumwa wa wenzao, na wakifikiria mambo ya wanadamu tu; yaani, “wananionaje,
wananisemaje, wanapendezwaje, n.k.”
Jambo hili limewafanya karibu watu wote kuishi maisha ya kuabudiana wao kwa wao, huku wakijibidiisha kufikia kile kiwango kilichowekwa na wenzao. Watu hung’ang’ania kupendwa, kukubalika na kuungwa mkono. Pia hujitahidi kujiepusha mbali na yale yawezayo kuwafanya wapuuzwe, hata kama ndiyo mazuri na ya haki.
MATOKEO YAKE
Baada ya watu kujipangia na kudumu katika huo mfumo ambao ndio huitwao “ulimwengu wa leo”, wanadamu wamefikia katika hali gani ya maisha? Amini usiamini, lakini ukweli ni kwamba; matokeo ya kuufuata huo mfumo wa wanadamu kuangaliana na kuabudiana wenyewe, ni hizi shida tunazoziona hivi sasa. Katika hizo jitihada za mtu kujiweka panapokubalika na wenzake, kumetokea
malumbano yasio na mwisho. Jamii zinazidi kuvunjika, serikali zinaendelea kupinduliwa, uongo umeongezeka huku kila mtu akijaribu kumnyang’anya mwenzake kwa namna moja ama nyingine; wizi wa mabavu, vita ambavyo vimewafanya watu kufa maji wakikimbilia kwenye usalama, vifo vitokanavyo na mangonjwa yasiyo na tiba, uchafuzi wa mazingira ambao umeleta mabadiliko ya hali ya hewa
yanayosababisha mafuriko, vimbunga vikali, na mengine mengi. Haya yote yanathibitisha wazi kwamba, huu mfumo, mila na tamaduni zake, una kasoro kubwa sana!
Ni kasoro gani hiyo? Tulianza kwa kusema kwamba, ulimwengu wa leo haujitambui; na sasa huo usemi unathibitishwa na haya matokeo mabaya ya maisha yasiyo na ufahamu. Haya matokeo yanazidi kuwa mabaya kila uchao mpaka watu wameanza kuyaona maisha kama yasiyo na maana kamili. Karibu kila mtu anaishi kwa woga na kutojua kitakachojiri baada ya kuona jinsi wengi wanavyoangamia na
wengine kupatwa na madhara mbali mbali kwa ghafla. Watu sasa wamebaki kushangaa na kujiuliza kama kweli kuna Mungu ambaye anayaona haya yote huku akikaa kimya bila kufanya cho chote ili kuokoa katika hali hii. Na ili tupate jibu sahihi, inatubidi tutafute chanzo cha huu mfumo na mwanzilishi wake.
Tutatafuta wapi basi? “Yuko Mungu mbinguni afunuaye siri” (Danieli 2:28), atatujulisha aliyeanzisha huu mfumo ambao umeleta maovu haya yote. Baada ya kumwuumba mwanadamu, Mungu alimwagiza kuhusu namna apaswavyo kuishi. Na hayo maagizo yahusuyo maisha ndiyo kile kupitia kwa manabii na mitume kiliandikwa kikawa ile biblia uisomayo leo. Kuhusu haya maagizo, muumba wetu anatuambia, “Wana amani nyingi waipendao sheria yako, Wala hawana la kuwakwaza” Zaburi 119:165. Je! hili si kinyume cha yale maisha tuyaonayo leo ya vita na vikwazo tele, kuthibitisha kwamba haya ndiyo maisha ya kweli? Anazidi kuthibitisha hayo akisema, “Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na afya ya mwili wao wote” Mithali 4:22.
Sasa basi, kwa mujibu wa haya maagizo ya Mungu muumba ambayo ndiyo maelezo sahihi kuhusu maisha; je! Mungu anasema kwamba mwanzilishi wa haya maisha maovu ya kutatanisha ni nani? Hebu tufuatilie tafadhali. Baada ya kumwambia Adamu haya maagizo ya maisha mazuri, Mungu pia alimuonya kuhusu maisha ambayo ni ya uharibifu, na ambayo yatamuua endapo akiyafuata. Sikiliza vile alivyomwambia, na ambavyo ndivyo pia akuambiavyo wewe leo usomaye ujumbe huu ikiwa unatafuta kuishi vizuri kwa Amani na furaha. Anasema: “walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika” Mwanzo 2:17. (kwa maelezo zaidi kuhusu huu mti, agiza ujumbe wetu usemao, “MITI MIWILI”, ili ujifunze zaidi, utatumiwa bure). Ukisoma Mwanzo 3:4-6, utaona kwamba mwanadamu alishawishiwa na Shetani, na akafanya kinyume na maagizo ya Mungu, akala yale matunda aliyokatazwa kula. Kwa hivyo sasa, tumepata jibu la swali letu; kwamba, aliyeanzisha haya maisha mabaya ya uharibifu si Mungu, bali ni Shetani. Alimwambia mwanadamu kwamba, Mungu aliye muumba wake amemdanganya. Lakini je! Shetani yeye alisema ukweli?
Mungu ambaye kama vile tulivyoona mwanzoni, ndiye peke yake ajuaye na afunuaye siri, anatuambia kuwa Shetani ni mwongo, maana anasema, “yeye (Shetani) ni mwongo, na baba wa huo” Yohana 8:44. Tena,“…aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote…” Ufunuo 12:9.
Haya yanazidi kuthibitisha kile tulichoanzia kusema kwamba, karibu watu wote leo hawajui cho chote kuhusu maisha. Na hii ni kwa sababu kile walichopokea na kukubaliana nacho kama mwongozo (ufahamu) wa maisha kutoka kwa Shetani ni uongo. Mungu akiyathibitisha haya anatuambia: “Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia: Hakuna mtenda mema, la! hata mmoja… Wala njia ya amani hawakuijua” Warumi 3:11-12, 17. Kutokana na huu ujinga, watu wanamlaumu Mungu kwa haya mabaya yote yanayoendelea. Wameendelea kulaumu hata kufikia kiwango cha kumwona Mungu kama mwenye upendeleo. Kama anayependelea kabila zingine zaidi ya zingine. Basi elewa sasa kwamba, si Mungu aliyeuleta huu uovu, bali ni Shetani, na ndiye
mwenye kuwafanya watu waoneshe huu upendeleo. (kwa maelezo ya kina zaidi, agiza ujumbe wetu usemao, “SHETANI NI NANI?”, ili ujifunze zaidi).
Sasa basi, tumejua chanzo cha ubaya na uovu wote uliyomo ulimwenguni leo. Tufanye nini sasa ili tujiepushe nao na tuweze kuishi maisha ya ushirikiano yenye Amani na furaha?
TUBUNI
Ukishajua kikulacho, kama mtu mwenye busara, utafanya nini? Utaendelea kushikamana nacho? Sio rahisi. Kile utakachofanya haraka iwezekanavyo ni kuachana na kitu hicho na kujitenga mbali nacho kabisa. Na hivyo ndivyo Mungu katika Kristo yesu anavyotuagiza akisema, “tubuni”. Neno “kutubu” lina maana ya, “kugeuka”, ama “kuacha”. Kwa hivyo basi, suluhisho ni kuacha kuishi kwa kuufuata
huu uongo wa Shetani, na tuanze kuishi kulingana na kile Mungu atuambiacho katika Maandiko. Na ili tufaulu kufanya hivyo, inabidi kwanza tuache kutumia akili zetu kujaribu kupanga mambo vile tunavyoonelea wenyewe, maana Mungu anawaambia wale waliotubu (waliogeuka kuachana na udanganyifu wa Shetani) kwamba, “Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili
zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako” Mithali 3:5-6. Hivyo basi, inatubidi kuanza upya kama watoto wachanga waliozaliwa hivi sasa. Lazima turudi kwa Mungu ili atuambie sisi ni nini, tunafanya nini hapa, na ni nini hatima (mwisho) ya maisha yetu? Majibu ya haya maswali ndiyo yaliyoandikwa na yakaitwa Biblia, yaani, Maandiko Matakatifu. (soma ujumbe
wetu usemao, “MWANADAMU NI NANI?”, kwa maelezo ya kina zaidi).
Kwa hivyo basi, muumba wetu anasema sisi ni nini? Naam; anasema, “BWANA Mungu akamfanya Mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai” Mwanzo 2:7. Kwa hivyo basi; Wewe ni mavumbi. Nani kasema? Je! ni sisi? Sio sisi tusemao hayo, bali ni yeye aliyekuumba, na ambaye peke yake ndiye akufahamuye. Ikiwa tutatubu (tutageuka), ni lazima tuanze kwa kukubali kwamba sisi ni mavumbi. Kwa mujibu wa uongo wa Shetani; ni kwamba wewe ni kama Mungu na wala wewe sio mavumbi; tena kwamba Wewe huwezi kufa, una roho isiyokufa ndani yako (soma Mwanzo 3:4-5). Hapa ndipo siri kubwa ya uongo wa Shetani ilipofichwa, na ndio chanzo cha uovu na uharibifu wote tunaoushuhudia ulimwenguni leo. Tunasema hivyo kwa nini? Maana baada ya kuukubali uongo kwamba sisi ni kama Mungu; basi kilichofuata ni sisi kujidhania na kujitumainisha kuwa tu wakamilifu na tusioweza kukosea, yaani tunaojua kila kitu. Kwa sababu hiyo, jirani yako anapokukosea; basi unasema kwamba anafanya makusudi, ni ujeuri tu. Tena
anapowezeshwa na Mungu kutenda wema; basi unasema ni mwenye hekima, anafaa kuabudiwa na kupewa sifa. Katika huu mfumo wa uongo, Shetani anahakikisha kwamba, hakuna kusameheana kabisa, bali ni kulipiza kisasi tu; na kwa njia hii, amewasha moto usiozimika duniani. Hii ndiyo sababu unaona umoja wa mataifa waking’ang’ana kuleta Amani; na badala yake,vita vinazidi kusambaa kila kona
duniani.
Lakini Mungu ambaye peke yake ndiye mkweli anasema kinyume na Shetani. Anatukumbusha kwamba hatujui cho chote, maana anatuambia kwamba; “Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu (yaani, atubu), ili apate kuwa mwenye hekima (kwa kuishi kwa maelekezo ya Mungu). Maana hekima ya dunia hii ni
upuzi (ni uongo na ujinga) mbele za Mungu… ” 1 Wakorintho 3:18-19. Ufahamu wa kweli wa kuhusiana na mwanadamu mwenzako anapotenda wema au ubaya ulioneshwa na bwana wetu Yesu Kristo ambaye ndiye Mjumbe tuliyetumiwa na Mungu kuja kutufundisha maisha halisi. Wakati watu walipomtendea mabaya, hata wakati walipokuwa wakimuua, yeye hakupigana kulipiza kisasi. Na badala
yake; alisema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo” Luka 23:34. Je! alikuwa akisema hivyo kwa kujifanya tu? La, hasha. Bali alimwamini Mungu kwamba, wanadamu wamedanganyika na hivyo wanauita wema kuwa ni ubaya, na ubaya kuwa ni wema.
Stefano ambaye alimwamini Yesu, aliyarudia maneno hayo hayo wakati alipokuwa akipigwa kwa mawe akisema; “Bwana, usiwahesabie dhambi hii” Matendo 7:60. Je! wote hawa walikua wakiongea hivyo kwa unafiki na kujifanya tu? Je! walikuwa wakiyanena hayo huku wakiwa na hasira na chuki nyingi dhidi ya hao watesi wao? Sivyo hata kidogo. Bali ni watu walioamini na kuyakubali yale Mungu
asemayo kwamba, “hakuna aliye na ufahamu, wala aliye mwema, maana bado hatujakamilishwa tukawa kama Mungu ambaye peke yake ndiye mwema na mwenye ufahamu wa kweli”, soma Matendo 19:17.
Pia, kwa habari ya kupokea sifa kutoka kwa wanadamu wasiofahamu kwamba ni Mungu ndiye amwezeshaye mtu kutenda wema; Yesu ambaye ndiye anayetufundisha maisha ya Mungu ya kweli, hakukubali sifa zimwendee yeye badala ya Mungu. Wanadamu walipomjia wakimwita mwema; aliwaambia, “Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake”, soma Mathayo 19:17. Alimaanisha nini? Alimaanisha kwamba, kama kuna mtu atendaye wema, basi huo wema amepewa na Mungu. Mtu huyo ni kama gitaa lichezwalo, na hivyo, sifa zinafaa zimwendee mcheza (au mpiga) gitaa na sio gitaa lenyewe.
Hili linathibitika kwa Paulo, alipotenda maajabu (miujiza) huko Efeso na watu wakataka kumwabudu (kumsifu). Yeye alikataa akawaambia, “Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamuhali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke (mtubu) na kuyaacha mambo haya yaubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo” Matendo 14:15. Na hata malaika wenyewe wanajua ya kwamba, ni Mungu peke yake ndiye anayefaa kusifiwa kwa kila jambo jema wanalofanya wanadamu. Yohana alipotaka kumwabudu malaika, aliambiwa, “Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu” Ufunuo 19:10. Je! hao nao walikuwa wanajua wayasemayo ama hawakujua?
Tangu lini watu wakakataa sifa? Watu hawa {akina Stefano, Paulo n.k.} walijua kwamba wao ni udongo (mavumbi) ambao bado uko katika mikono ya mfinyanzi. Kwa hivyo basi, cho chote kile kilicho chema kinachotendeka maishani mwao, ni mfinyanzi (muumbaji) ndiye atendaye na wala sio wao. Walijua vizuri sana kwamba, sisi wanadamu wa kimwili sasa hivi hatuna uwezo wa kutengeneza ufahamu. Akili zetu hutegemea kujifunza kutoka kwa Mungu au kwa Shetani. Naam, ukweli ni kwamba; ufahamu wetu hutokana na mafundisho yatokayo katika ulimwengu wa roho, ambapo kila mwanadamu anajiunga kufundishwa ama na Mungu au na Shetani; na hivyo, anakuwa mtumwa wa yule amfundishaye. Wema ni wa Mungu, na ubaya ni wa Shetani. Na hii ndiyo maana, badala ya kumlaumu anayemtumikia Shetani
atendapo ubaya; wanamhurumia mtu huyo, maana wanajua kuwa yeye ni mtumwa. Maana imeandikwa: “Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki” Warumi.6:16. Hii ndio sababu pia, mtu alipotenda mema, walijua
kwamba ni Mungu ndiye atendaye ndani ya mtu huyo, na hivyo walimsifu Mungu; yaani, walikataa “kuabudu kiumbe badala ya kumwabudu yeye aliyekiumba”, soma Warumi 1:24. Unaona sasa jinsi ambavyo ulimwengu umechanganyikiwa, na kwamba badala ya kufuata maagizo ya Mungu ili waishi vizuri kwa Amani; wanafuata uongo wa Shetani huku wakitumia fikira na mawazo yao wenyewe? (kwa maelezo zaidi, agiza ujumbe wetu usemao, “UJUZI WA MAWASILIANO”, ili ujifunze zaidi, utatumiwa bure ujumbe huo).
Wapendwa wetu; huku kutojijua, pamoja na watu kuukubali uongo wa Shetani na kuutumia kama ufahamu wa maisha, ndiko kumeleta hizi vurugu zote tunazoziona duniani leo. Wakijidhania kujua na kujichukulia kuwa kama miungu, basi kila mmoja anang’ang’ana na kupigana na mwenzake, aitha akitaka kusifiwa, ama akipinga kudharauliwa. Ni kweli kwamba, Mungu alituahidi kutufanya kuwa
miungu; lakini kwa sasa, sisi ni mavumbi. Ni mpaka pale ambapo tutakamilishwa; lakini kwa sasa hivi hatuna cha kusifiwa wala kulaumiwa, maana kwa sasa sisi ni watumishi wa wema wa Mungu au wa ubaya wa Shetani. Hii ndiyo sababu Mungu anatuambia kwamba, “kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama (yaani, si dhidi ya wanadamu); bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” Waefeso 6:12.
Tufanye nini basi? Tutubuni (tugeukeni), tuache kuutumia uongo wa Shetani, na badala yake, tuanze kuutumia ukweli wa Mungu kama ufahamu wa maisha mema na makamilifu. Tuache kabisa kujidanganya kuwa tunajua; na badala yake, tuanze upya kabisa, maana Mungu anatushauri kwamba, “Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu (yaani, akubali kwamba hujui cho chote), ili apate kuwa mwenye hekima (kwa kujifunza kwa Mungu)” 1 Wakorintho 3:18. Naam; tukubali kwamba kile tulichokitumia miaka yote hii kama ufahamu wa maisha ni uongo. Kwa hivyo sasa, ni juu yako wewe unayeusoma ujumbe huu kufanya uamuzi. Je! utaendelea kuishi kwa kuufuata uongo wa Shetani uliokudanganya kwamba wewe ni
kama Mungu, ama utaukataa tangu sasa na uanze kujifunza kwa Mungu ukweli ambao Mungu atautumia kukuumba akili na mawazo yako ili yawe kama yale yake, na mwishowe akufanye kuwa kiumbe wa kiroho kama yeye? Kama unataka kujifunza ukweli; basi Mungu anakuambia uanze kwa kufahamu kwamba, “wewe ni mavumbi (udongo), na wala sio Mungu”, soma Mwanzo 3:19. Na tena ufahamu
kwamba, “wewe ni kama nyasi, na maisha yako ni kama maua ambayo hunyauka baada ya muda mfupi tu”, soma Isaya 40:6-7. Na zaidi ya hayo, ujue ya kuwa, “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu”, soma Ayubu 14:1-2. Ikiwa utakubaliana na hayo; basi sasa wewe uko tayari kuanza upya kijifunza kwa Mungu. Naye Mungu anasema tufanye nini baada ya kuyakubali hayo?
THAMANI YA MAVUMBI
Wale wote waliotangulia mbele yetu ambao walimwamini Mungu na kuanza kujifunza kwake, katika maandiko wanashuhudia ukweli huu. Ibrahimu ambaye Yesu Kristo alizaliwa kutokana na uzao wake, alitambua na kukiri akisema, “… nami ni mavumbi na majivu tu” Mwanzo 18:27. Daudi ambaye alishuhudiwa kuwa na roho kama ile ya Mungu anasema, “Kwa maana Yeye (Mungu)anatujua umbo letu, Na kukumbuka ya kuwa sisi tu mavumbi” Zaburi 103:14. Nabii Isaya anathibitisha huu ukweli wa Mungu akisema, “… sisi tu udongo… sisi sote twanyauka kama jani” Isaya 64:8,6. Paulo naye anaongezea kasema, “Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema”Warumi7:18.
Baada ya kuupata huu ukweli wote kutuhusu sisi wanadamu; sasa basi, hebu tuone ile siri ya udanganyifu wa Shetani inavyofanya kazi; na ambayo ndiyo sababu Mungu anawaagiza wote watakao kutoka katika huo uongo wajikane kwanza nafsi zao na kuachana kabisa na mwenendo wa awali.
Ni kitu gani katika mavumbi ambacho ni cha thamani kiasi kwamba utakitetea na kukishikilia? Mavumbi yako kila mahali. Tunayakanyanga, tunayatupia takataka, vinyesi n.k. Siku moja, nilitembelewa na marafiki zangu nyumbani kwangu. Na walipokuwa wakitembea hapa na pale; hili wazo la mavumbi likanijia akilini. Niliwaangalia wakiyakanyanga mavumbi na wala hakuna aliyekuwa na haja nayo.
Nikajiuliza; “kama haya mavumbi yangekuwa ni dhahabu ama almasi, je! kila mtu asingekuwa anang’ang’ana sana kuokota kulingana na uwezo wake? Lakini sasa, kwa vile ni mavumbi tu; basi hakuna mwenye haja nayo”. Je! nayaongelea mavumbi? La, hasha; bali naongea kuhusu sisi wanadamu. Hivyo ndivyo tulivyo katika haya maisha yetu ya kimwili. Hatuna thamani yo yote ile ya kutamanika wala kupiganiwa. Lakini kinyume cha huu ukweli; watu kila mahali ulimwenguni wanapigana kila mmoja akitetea msimamo wake. Kwa nini? Kwa sababu uongo wa Shetani unatuambia kwamba sisi ni kama Mungu, na kwa hivyo mtu asituone wajinga, wala asitufikirie kuwa wanyonge n.k.
Ni kwa nini hatuangalii mfano wa wale wapatao ajali za barabarani, au za milipuko ya mabomu, au athari ya kukosa vyakula ama maji? Je! hatuoni jinsi wanavyotawanyika kama mavumbi tu? Ku wapi kule kuwa kama Mungu? Ki wapi kitu cha kupigania katika huu mwili unaotawanyika na kuvunjika kama mayai? Ki wapi kitu cha kutegemea katika utajiri ambao hautupi uhai? Je! utajiri unaweza kutulinda dhidi ya madhara hayo pindi yatupatapo?
Hapa ndipo siri ya uongo wa Shetani ilipo. Tumeacha kutafuta ile thamani ambayo Mungu alituahidi (yaani, kutokufa na miili isiyoharibika),na badala yake tukakubaliana na Shetani na tukaanza kujiharibu huku tukidhani kuwa tunajijenga. Tunapaswa tugutuke (tuamke) na tujue kuwa Shetani anataka tujimalize wenyewe; naam, anataka tufe sote kwa kuufuata huo uongo wake. Ili tujitoe hapo, ni lazima tukubali kwamba sisi ni mavumbi, na tumwendee Mungu ili aendelee kutuumba hata tufikie kiwango cha kujivunia na cha kutetea. Lazima pia tukubali kwamba haya maisha ya uongo wa Shetani ndiyo ambayo yanasababisha huu uovu wote uliomo duniani sasa.
Kama kila mtu duniani angejikubali kuwa yeye ni mavumbi, na kumwendea Mungu ili aumbwe upya, je! watu wangetofautiana ama kupigania nini? Kama kila mtu angekuwa mwangalifu asidanganywe na Shetani na badala yake amfuate Mungu, je! tofauti kati yake na mwanadamu mwenzake ingetoka wapi? Kwa hali hiyo wapendwa: je! dunia isingekuwa na Amani na furaha isiyo na kifani?
Tumshukuru Mungu ambaye kwa upendo wake kwa wanadamu, aliyaona haya mateso yote, na akamtuma mjumbe wake Yesu Kristo ili aje “atufungue macho ili tutoke katika huo uongo na kuja katika ufahamu wa kweli, tutoke kwenye uharibifu na kuuendea uzima, ili Amani mwishowe iijae dunia yote”, soma Waefeso2:17-18.
MGEUKIE MUUMBA WAKO
Tuanzie wapi basi? Tuache kuangaliana na kutafutana sisi kwa sisi; na badala yake tuanze kumwangalia na kumtafuta Muumba wetu ambaye ndiye pekee atakayetuambia ukweli wote kutuhusu. Watu kwa kutokuyafahamu hayo, wameyaacha mafundisho ya Mungu na kujidhania kuwa wenye hekima, ambayo matokeo yake ni kinyume. Mungu anawashangaa akiuliza: “Mwasemaje, Sisi tuna
akili,… tazama, wamelikataa neno la Bwana (ambalo ni maisha ya kweli), wana akili gani ndani yao?” Yeremia 8:8-9. Na tena: “… ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili (sheria za Mungu), bila shaka kwa hao hapana asubuhi (ni giza na ujinga mtupu)” Isaya 8:20. Ikiwa basi tunataka kujiepusha na haya maovu na kupata ulinzi kutoka kwa muumba wetu, basi anatuambia; “Mimi ni Bwana, Mungu wako,
nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari” Isaya 48:17. Je! tunayaamini haya Mungu ayasemayo hapa? Na kama ndiyo; basi tuanze kwa kujisahau, kuwasahau wanadamu wenzetu, kusahau mila na tamadumi zote ambazo zimejengwa juu ya uongo;
ambazo kadiri tunavyong’ang’ana kuzitimiza ili tupate kibali mbele ya wanadamu, tumejiletea shida ambazo sasa zinatishia kutumaliza. Mungu anasema tukubali kwamba, “Baba zetu hawakurithi kitu ila uongo, naam, ubatili na vitu visivyofaa. Je! Mwanadamu ajifanyie miungu, wasio miungu?” Yeremia 16:19-20. Naam; wanadamu walianza kwa kumweka Mungu kando na wakaanza kuangaliana wao kwa
wao na kuabudiana huku wakitegemeana, jambo ambalo Mungu amekataza kabisa akisema; “Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana” Yeremia 17:5. Anazidi kuonya akisema, “Maana BWANA aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema, Msiseme, Ni fitina; katika habari za mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni fitina; msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. BWANA wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu” Isaya 8:11-13. Endapo tutayasikiliza haya maagizo na kuyatii; basi tutaacha kubabaishwa na maneno ya wanadamu na kuacha pia kuyategemea kama hukumu zetu, iwe ni kwa kusifiwa ama kwa kudharauliwa. Maana, ikiwa tunajua vizuri kwamba mtu hana ufahamu wo wote; basi wakati anapokudharau au kukusifu, yote hayo ni udanganyifu tu. Sasa kwa nini utegemee hukumu zake badala ya kutegemea hukumu za Mungu katika maandiko? Mungu anatuuliza akisema; “Mimi, naam, mimi, ndimi niwafarijiye; wewe u nani hata ukamwogopa mtu atakayekufa, na mwanadamu atakayefanywa kuwa kama majani? Ukamsahau BWANA, Muumba wako, yeye aliyezitanda mbingu, na kuiweka misingi ya dunia; nawe unaogopa daima mchana kutwa kwa sababu ya ghadhabu yake yeye aoneaye, hapo afanyapo tayari kuharibu; nayo i wapi ghadhabu yake aoneaye?” Isaya 51:12-13.
Ikiwa mtu haongei maneno ya Mungu; basi asikubabaishe kwa lo lote, iwe kwamba anakusifu ama kwamba anakudharau, maana anaongea uongo, na tunajua kwamba uongo ni ubatili. Yesu aliyajua hayo na ndiyo sababu alisema kwamba; “Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu (kwa ajili ya maisha ya kweli). Furahini siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni…” Luka 6:22-23. Tena wakati wanapokusifu (kwa kutokujua kwamba ni Mungu ndiye atendaye wema ndani ya wanadamu: soma Wafilipi 2:13) kwa sababu umetenda yale wayapendayo, je!
ufurahie na kukubaliana nao? Na isiwe hivyo. MaanaYesu anatuambia; “Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo” Luka 6:26.
Kwa nini? Kwani ni vibaya kusifiwa? La, hasha. Lakini uelewe kwamba, mwanadamu wa kimwili husifu tu kile kimpendezacho; na kile kimpendezacho ni ule uongo wa Shetani. Kwa hivyo; mara nyingi, ukiona wanakusifu na kukushangilia, basi ni kwa sababu unafanya mapenzi yao. Kwa maana, ikiwa ni watu wanaomjua Mungu na kusifu kwa haki; basi hawatakusifu wewe bali Mungu. Yesu anayashuhudia hayo akisema; “Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu” Luka 16:15: soma pia Wakorintho 10:12; Yohana 5:44.
Kwa hivyo; endapo tutafaulu kujiepusha na huu mpango mbaya wa maisha, tukaanza kwa kujikubali kwamba, sisi ni mavumbi, ni udongo ulio mikononi mwa mfinyanzi (Muumbaji) ambao anaufinyanga ili aweze kumtengeneza mtu aliyetukuka na wa kiroho kama Mungu mwenyewe; tukishajiweka katika hali hiyo, hatutakuwa na cho chote katika huu mwili ambacho tunaweza tukakitetea.
Tutavipuuza vyote vya kimwili na kutia jitihada zetu zote katika kuishi kama Mungu na sio kwa kuwaiga wanadamu wenzetu au tamaa za mwili za uharibifu na za kudanganya(soma Waefeso 4:22).
Ni ndani ya akili za wanadamu ambako vita hupangwa na kuanzia (soma Yakobo 4:1-2). Na kwa hivyo pia, ni hapo ndani ya akili ndipo ambako msingi wa ujenzi wa Amani utakapowekwa. Unahitaji mabadiliko ya nia (akili) na mawazo(mtazamo)ili mabadiliko ya mipango na utendaji pia yafanyike. Huu ndio ujumbe ambao Yesu anawafundisha wote wanaomwamini. Hii ndio habari njema aliyotuletea kutoka
kwa Mungu muumba wetu, na ni kwa ajili ya wanadamu wote. Sasa je! kwa vile tumeyafahamu haya, tuko tayari kubadilika? Je! tuko tayari kuutupilia mbali huu ufahamu wa zamani wote, na kama watoto wadogo, tuanze kujifunza kwa Yesu katika maandiko? Na kama ndiyo; basi hatua ya kwanza ni kutoa mawazo yetu kutoka kwa wanadamu, na kutoka katika mila na tamaduni zao, na tuyaelekeze kwa Mungu
aliyetuumba ambaye ndiye peke yake ayafahamuye maisha ya kweli. Tukiishafanya hivyo, hili litabadilisha kila kitu katika maisha yetu. Yale malengo ya kujitahidi kufanya yale ambayo wanadamu wanayataka ili wakupende, ile hali ya kufanya kila kitu kwa kujitazama au kumtazama mwanadamu mwenzako na kuishi kulingana na mila zao, itaondoka. Lengo litakaloanza kutuongoza maishani litakuwa
ni lile la kutaka kuufikia uzima wa milele na kufanywa kuwa viumbe wa kiroho kama Mungu.
Tukijiweka kwenye hali hiyo, hatutakuwa na kitu cha kung’ang’ania kati yetu. Hatutakuwa na sababu ya kuchukiana au kupigana, maana tutatambua kuwa adui yetu sio mwanadamu mwenzetu, bali ni Shetani aliyemshika mateka kutenda mapenzi yake; na tutaweza kukubaliana na Mungu anavyotuambia kuwa, “vita vyetu sio dhidi ya damu na nyama (mwanadamu), bali ni dhidi ya pepo wabaya
(mashetani)“, soma Waefeso 6:12. Tutafikia katika kiwango cha kutii agizo la Yesu atuambialo kwamba, “Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo… Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi” Mathayo 5:42,44. Katika hili lengo jipya la maisha, na katika hii akili mpya, utaona kwamba; tabia za wizi, uasherati, unyang’anyi, tamaa mbaya, chuki na mauaji zitaisha.
Na kufikia hapo rafiki; je! wewe huoni kuwa hii akili mpya ambayo ulimwengu wa leo haunayo ndiyo suluhisho la shida zote zilizoko duniani leo? (kwa maelezo mengine zaidi, agiza ujumbe wetu usemao, “MWANADAMU NI NANI?”, ili ujifunze zaidi). Je! huoni kuwa ni kinyume cha ile akili iliyopo hivi sasa? Tukubaliane kwamba, ni Shetani kupitia kwa hii akili ya sasa ya uongo ambaye anawafanya wanadamu kutenda haya maovu yote. Yeye Shetani hatafuti wafuasi, bali anataka kuwadanganya wanadamu, na kwa njia hiyo awafanye kuyakataa maisha ya kweli ili wafe wote. Hii ndiyo sababu unaona wanadamu wanauana kama wanyama; wanatengeneza vitu ambavyo ni hatari sana kwa mazingira. Yote haya ni jitihada za Shetani za kutumaliza kwa kututumikisha kwenye hii akili yake ya udanganyifu. Angalia matokeo yake sasa hivi. Kila taifa duniani leo linakabiliana na upinzani wa aina moja ama nyingine. Vita vinavyosababisha maafa ya maelfu elfu ya watu viko kila mahali. Naam, huyu ni Shetani akitekeleza lengo lake.
Hii ndiyo sababu Mungu kwa huruma zake, ameyaona haya na akaamua kumtuma Yesu, ili atufumbue macho tupate kuiona hii siri ya uongo wa Shetani. Yesu anatukumbusha kwamba, tuko katika huu mwili ili tujifunze kuishi kama Mungu huku tukiyakataa mafundisho ya Shetani, ili kusudi tukishakamilika, tupate kuvikwa miili ya kiroho na kisha tuurithi ufalme wake. Ndiyo sababu alianza kwa kusema, “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili” Marko 1:15. Kwa wale watakaousikia wito huu na kuuamini, Mungu anaahidi kuanza kuumba akili yake ndani yao kwa kuziandika amri zake ndani ya mioyo yao ili ziwe ndizo mawazo, fikira na nia za mioyo yao, naam; ziwe ndizo ufahamu wa kutenda cho chote kile mtu atakachotenda katika maisha. Na hili atalifanya
kwa kuwapa roho yake takatifu itakayowawezesha kuyakumbuka haya maagizo yake. Amewaahidi pia ulinzi wake, maana anasema, “BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele” Zaburi 121:7-8. Ni kwa kuishi kulingana na hii akili ya Mungu ndiko ambako kutaleta Amani, na ni baada ya kuwa akili zote za wanadamu
zimeigeukia katika wakati ule ambao ufalme wa Mungu utaanza kuitawala dunia hii, na huku pia Shetani akiwa ameondolewa. Kuhusu wakati huo ujao, Mungu anasema, “Miisho yote ya dunia itakumbuka, Na watu watamrejea BWANA; Jamaa zote za mataifa watamsujudia. Maana ufalme una BWANA; Naye ndiye awatawalaye mataifa”, soma Zaburi 22:27-31.
Wapendwa wetu; hili ndilo tumaini la wanadamu. Na hii ndio njia pekee ya kuleta Amani duniani; ni kwa kuimarishwa kwa ufalme wa Mungu, na kuondolewa kwa Shetani ambaye kwa sasa hivi ameushika ulimwengu mateka akijaribu kutekeleza ndoto yake ya kuwaua wanadamu wote. Kuhusiana na wakati huo ujao, Mungu anasema: “Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu
mlimani kwa BWANA, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake…” Hebu na tulifahamu jambo hili hapa kwamba; baada ya kila mmoja kuanza kujifunza kuishi kama asemavyo Mungu; wakati ambapo serikali ya Mungu itakuwa imeimarishwa, na mji wake mkuu ukiwa Yerusalemu; naam, wakati ambapo “sheria itatoka Sayuni, na neno la BWANA kutoka Yerusalemu” huku BWANA mwenyewe “akiwahukumu mataifa”, je! kutatokea nini? Nia na mawazo ya watu yatabadilika, “.…nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena
kamwe” Isaya 2:3-4. (kwa maelezo ya kina zaidi, basi agiza kitabu chetu kisemacho,“UFALME WA MBINGUNI”,ili ujifunze zaidi).
Sasa je! mpendwa; Wewe ni miongoni mwa wale wanaoitafuta hii Amani ya kweli, na ungependa kuwa miongoni mwa wale wanaojitayarisha kwa ajili yake? Wajumbe wa Mungu wako hapa tayari kukujulisha mengi. Na huduma hii inatolewa kwako bure kabisa pasipo malipo yo yote yale utakayotozwa. Ni kazi ya Mungu na wala si ya mwanadamu. Unachohitaji kufanya ni kuwasilina nasi
kwa anuani zetu zilizopo hapa chini, nasi tutakuhudumia bure.
Tunavyo vijarida na vitabu vingi na vyenye mada mbali mbali vitolewavyo bure kwa ajili yako. Baadhi ya vijarida vyetu ni kama vile;
- JE, WEWE NI MKRISTO?,
- KUOKOLEWA KWA NEEMA,
- KWANINI SHERIA?,
- THAMANI YA UKRISTO,
- KANISA LA SIKU ZA MWISHO,
- JE! KRISTO
- AMEGAWANYIKA?,
- SHERIA ZA KIAFYA,
- ROHO YA SABATO ZA MUNGU,
- MWANADAMU NI NANI n.k.
Baadhi ya vitabu vyetu pia ni kama vile;
- UFALME WA MBINGUNI,
- KIFO NA KIYAMA,
- SIKUKUU ZA MUNGU,
- AMRI KUMI,
- DINI ZA MITINDO,
- BIBLIA NA AFYA ZETU,
- KUFA NA KUFUFUKA KWA YESU,
- MISINGI YA IMANI YA KANISA LA MUNGU n.k.
Agiza sasa kile/vile utakavyopenda kujifunza, nasi tutakutumia huko ulipo bure kabisa. Wasiliana
nasi kwa anuani zifuatazo:-
KANISA LA MUNGU – TANZANIA
Nambari za simu; +255 753 359 179, +255 688 359 179 na +255 655 659 179
Barua pepe; Ukweliwabiblia@yahoo.com.sg
KANISA LA MUNGU – KENYA
Barua pepe; endcog@gmail.com
Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Utukufu una yeye tangu milele, sasa na hata milele; Amina.