Kunazo aina mbili za ufahamu katika akili za wanadamu ambazo wanazitumia kuishi vile wanavyoishi. Hizi fahamu ni tofauti na zinapingana. Kwa hivyo, haziwezi kutumika zote kwa wakati mmoja. Mungu alituumba tukiwa na uhuru wa kuchagua moja kati ya hizi mbili. Ni ufahamu ule mtu anaochagua ambao anautumia kufikiria, kuwaza, kupanga na kutenda kama namna yake ya maisha, maana, kwa yule mnayejitoa kwake kuwa watumwa kumtii, huyo ndiye mnayemtumikia-Warum.6:15-16. Ulimwengu wa leo umejengwa juu ya aina moja ya hizi fahamu mbili, na sisi zote tumewahi au, bado tunaendelea kuishi kwa kuufuatilia huo ufahamu- Waef.2:3. Ni aina ya ufahamu ambayo inawaacha wanayoishiriki, wakiishi, kutenda, na kufanya bidii zao zote, katika hali ya kushindana na kupingana, mtu na mwenzake-Mhubiri.4:4. Ni maisha ambayo, ijapokuwa wale wanaoyaishi wanaamini kuwa kunaye Mungu aliyewaumba, hawamtambui wala kumshirikisha inapokuja wakati wa mipango yao na utekelezaji wake.
Hii ni kwasababu, aina hii ya ufahamu ni ya kiwango cha kimwili peke yake, na, haiwezi kuyaelewa mambo ya kiroho, akiwemo Mungu, maana yeye ni roho- 1 Wakor.2:14; Yohana.4:24. Ni kwa nini basi wenye huu ufahamu wanajionyesha kumtambua Mungu, huku wakikataa kuyasikiliza maneno yake, na badala yake, wanafuata ushupavu wa mioyo yao wenyewe-Yerem.13:10? Ni kwasababu, hali watu wakiwa viumbe wa nyama na damu, na wasio na ufahamu wowote, na wenye uwezo wa kuyafahamu ya kimwili tu, walidanganyika kuwa, wao ni kama Mungu, hivyo basi, wanajifahamu kuwa wakamilivu, kumaanisha wanao ufahamu wa mambo yote- Mwa.3:4-5. Kwa hivyo, walibaki kuweza kujipatia ufahamu wa vitu vya kimwili, maana ndivyo akili zao ziwezao kuelewa– 1 Wakor.2:14. Mungu ni Roho- Yohana. 4:24, na shetani ni roho pia- Waef.2:2.
Kwa hivyo, ni jambo la kuaminika kwamba, mwanadamu wa kimwili hawezi kumwona, wala kumfahamu Mungu au Shetani, asipopokea roho nyingine ambayo inaiwezesha roho ya akili yake kuona na kuelewa kiroho. Tumesikia mara nyingi, watu wakihuzisha matukio na vitendo vyao, na Mungu au Shetani. Katika hiyo hali ya upofu, kila mtu amejipatia hali ya kuamua ni kipi atakochohuzisha na Mungu au Shetani. Nje ya ufahamu, wanadamu wanautumia uhuru walioumbwa nao, kutenda, kila mmoja kulingana na vile moyo wake unavyotamani-Yerem.18:12. Wapenzi, huu ndio ufahamu ambao ulimwengu wa leo umejengwa juu yake, na ambao wanadamu wote isipokuwa wachache, wanautumia kama namna ya kuishi.
TABIA ZAKE
Kabla hatujaendelea, tunapaswa kila mmoja kukumbuka kwamba, huu ufahamu ni wa Shetani, ambaye ameudanganya ulimwengu wote-Ufu.12:9. Tunaelewa pia kwamba mtu adanganyaye huwa nia yake, si ya kusaidia au kujenga mtu, mbali, ni ya kumnyima kilicho chema, akilenga kumwangamiza. Kristo anayathibitisha haya kuhusu Shetani anaposema kuwa, yeye ni mwizi, na amekuja kwa kusudi la kuiba na kuharibu-Yohana.10:10.Anazidi kumsema Shetani kuwa ni muongo na muuwaji-Yohana.8:44. Basi, ni wazi kwamba, huu ufahamu ni wa kumwangamiza mwanadamu, na ndio sababu, baada ya Kumuumba Adamu, Mungu alimuonya kuwa, akidanganyika kuufuata huo ufahamu, hakika atakufa-Mwa.2:17.
Katika Maisha haya ya kimwili, mwanadamu sio mkamilivu. Kwa hivyo hawezi kujitegemea kuishi bila msaada wa Mungu, maana, kama vile tawi haliwezi kuishi bila shina, na ndivyo mwanadamu hawezi bila Mungu-Yohana.15:4-5. Hii ni kwasababu, Mungu bado anaendelea kumuumba, na nafsi na pumzi ya kila mwanadamu I mikononi mwake- Ayubu.12:10. Ina maana kwamba, pasipo Mungu, bidii zote afanyazo mwanadamu ni za kumharibu-Zab.127:1. Mungu anayathibitisha hayo anapozidi kusema kuwa, roho ya Mungu ilimuumba mwanadamu, na pumzi zake umpa mwanadamu uhai-Ayubu.33:4.
Kinyume na huo ukweli, watu katika ulimwengu wa leo wamedanganyika kuwa wanaweza kupanga Maisha yao mazuri kama ya Mungu bila kumtegemea, kwa vile wako kama yeye-Mwa.3:4-5. Na kwa vile katika huu mwili, ni lazima mwanadamu ategemee mzaada wa kuishi kutoka kwingine, na amekataa msaada wa kipekee ambao ni Mungu aliyemuumba, basi, amebaki kutegemea nguvu na mali yake, na wanadamu wenzake. Basi, huku kila mtu akijibeba kama mungu, na akiwa ni lazima ategemee watu na vitu, hii hali imezaa Maisha ya ushindani miongoni mwa wanadamu, huku kila mmoja akijionyesha kuwa ndiye.
Huu ndio mwanzo wa furugu zilizoko duniani leo, maana kila mmoja anamtazamia mwenzake kwa msaada fulani, huku kila mmoja pia akijiona kuwa mkuu( mungu), na aliye bora kuliko mwenzake, ijapokuwa ni uongo ( soma ujumbe uitwao, “ Viwango vya wanadamu”, kwa maelezo Zaidi). Basi, wandugu, hapa ndipo lengo la Shetani linaanza kutimia maana, watu wanaoneana kila mtu na mwenzake, na kila mtu na jirani yake; mtoto anajivuna mbele ya wazee, na mtu mnyonge mbele ya mtu mwenye heshima-Isa. 3:5.
Rafiki zangu, kweli je,hii sio ile hali iliyoko ulimwenguni sasa, na ambayo imezaa vita na mauwaji kila mahali, na kuwaacha wanaoponyoka wakikaa katika hali ya taabu kubwa? Si ni kweli, Shetani amefaulu kwa kiwango fulani kuwauwa mamilioni ya wanadamu, kwa njia ya kuwapa hii akili idanganyayo, ambayo wanaitumia kufanya haya maovu yote? Haya yote yanafanyika, kwasababu mwanadamu amedanganyika kujiondoa kwenye mpango wa uumbwaji wake ( soma ujumbe, “mchakato wa uumbwaji wa mwanadamu”), na kwenye ile njia peke yake, yenye ulinzi na uimarishaji wa uhai.
Mungu alionya kuhusu huu wakati tunaoishi akisema, watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, watukanaji, wasiotii, wasio na shukrani, wasiopenda, wasiotaka suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wagaidi,wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu….. 2Timoth.3:1-4. Tukiangalia hapa, ni wazi kwamba, hawa watu hawajali kabisa vile wenzao watasikia wakiwafanyia hayo, na haya yote wanafanya pasipo kujali kwasababu, hawajijui, wala kuyajua Maisha wanayopaswa kuishi au, kujua tegemeo lao lilipo- Yohana.15:21. Katikati ya huu uovu na maudhi yote, Mungu anatuambia tutende mambo yote bila kunung’unika wala mashindano, maana kwa njia hii, tutathibitisha kuwa sisi ni wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wala ila, katikati ya kizazi kikaidi, na kilichopotoka, ili tuwe mfano (nuru) wa yale Maisha Mungu aliumba watu wote waishi kwayo- Wafilip.2:14.
Haii! Itawezekanaji kukosa kunung’unika, na kujitetea wakati watu wanatuthulumu pasipo sababu?
TUJIELEWE UPYA
Aitha, tutakubali kwamba, tulirithi uongo, na tukubali kuuwacha-Yerem.16:19, na kama watoto waliozaliwa sasa hivi, tukubali kufundishwa upya na muumba wetu-Mat. 18:2; 1 petro.2:2, au,la sivyo, haitawezekana kamwe kutolalamika na kunung’unika huku tukijaribu kujitetea na kupigania kile tutaita haki yetu, ilhali ni uongo. Huu ujumbe ni kwa wale wamefikia huu uamuzi, au wanaendelea kutafuta kuelewa na kuufikia. Kwa vile basi sisi ni wale tumekubali kuwa, tulichorithi kama ufahamu ni uongo, na tumekuja mbele ya muumba wetu, mbele ya mlimani mtakatifu wa Mungu wa Yakobo ( zayuni ya mbinguni-waeb.12:22), ili atufundishe njia za kweli, ili tuweze kuishi kwazo-Isa.2:3, hebu basi tutoe ufahamu wote wa zamani usiotokana na neno la Mungu- Waef.4:22, na tuanze upya. Tujiulize basi.
Ni kitu gani tunapaswa kutetea, kulinda, kusimamia na, kushughulikia kwa nguvu na mioyo yetu yote? Hakiwezi kuwa kinginecho isipokuwa uhai, na yale Maisha ya kuuendeleza, maana kristo anasema, ilipo hazina ya mtu, ndipo moyo wake huwa, na palipo moyo, hapo ndipo ulinzi wote unawekwa- Mat.6:21. Hiki ndicho kitu cha pekee kipasacho kutufanya tunung’unike, tupigane, na kushindana, yaani, kile tunachothamini kuliko vyote. Hivyo basi, Mungu anatuambia kuwa hicho tunachopaswa kuthamini kupita vyote ni nini? Ni kile ulicho ( ujumbe wetu, “wewe ni nini?”, unao maelezo Zaidi). Kinyume na vile tumezoea kujijua na kujibeba, Mungu anasema kuwa sisi ni mavumbi, kama nyasi na kama kivuli, huku Maisha yetu yakiwa kama ua la kondeni, ukungu, au pumzi, yaani, ya muda tu, na yenye matatizo chungu nzima-Mwa.3:19; Yakubu.4:14; Isa.40:6-7; Ayubu.14:2-3. Na ni Mungu mwenyewe alituumba tukiwa hivyo.
Kwa nini akatuumba katika hali hii isiyofurahisha, na yenye kuogofya? Najua wengi wetu hatutaelewa, lakini yeye mwenyewe anasema kuwa hii hali ni kwa ajili ya wema wetu; eee, kwa ajili ya faida yetu-Warum.8:28. Wandugu, ijapokuwa ni hali ya kutatanisha, Mungu anakusudia liwe la kufurahisha na kutumainisha,na hii itawezekana tu kwa wale watajifunza kwake na kujikubali hivyo. Basi je, Mungu anasema kunao wema gani katika huu unyonge, na tunawezaje kuufurahia?
KIWANDANI CHA UUMBWAJI
Mungu ni mkamilivu katika kila hali, na, niwa milele. Kwa hivyo amekomaa katika uzuri na utukufu usioweza kueleweka kwa hizi akili zetu ndogo. Wakati akituumba, alitaka, na mpaka wa sasa, anataka mwanadamu mkamilivu kama yeye-Mwa.1:26. Kama vile mjenzi uanza ujenzi wake kwa kuchora ramani ya huo mjengo, na vivyo hivyo, Mungu alianza uumbwaji wetu kwa mchoro, maana anasema, macho yangu yalikuona kabla hujakamilika, chuoni (kitabuni) mwangu, sehemu zako zote ziliandikwa, kabla hazijawa bado-Zab.139:16. Inatupasa basi kukubali kwamba, utaratibu wote wa uumbwaji wetu ndio Mungu anaotuelezea kupitia kwa maandiko.
Katika hayo maandiko, anatuambia kwamba huu mwili tulionao sasa, na Maisha yake, ni hatua ya kwanza ya kutuumba, na ni wakati wa kuumbwa ufahamu na tabia- yaani, wakati wa kusoma na kuzoea kuyatumia hayo masomo kama tabia, maana kama tulivyoona, maandiko ni maelezo( mchoro, ama, Ramani) ya vile tutaumbwa ata tuufikie ukamilivu. Mfano wetu wa kipekee wa zile hatua tutapitishwa hata kuufukia huu ukamilifu ni kristo. Basi, yeyote ambaye anataka kuumbika hata akamilike, ni lazima aige kwa kila namna, mienendo yote ya kristo, bila kupunguza, wala kuongeza kitu- 1 Yohana.2:6.Tunaambiwa kuwa, katika Maisha yake ya kimwili, Kristo alivumilia mateso(msalaba), akaipuuza aibu kama njia ya kuufikia ukamilifu-Waeb.12:2.
Kwa nini avumilie, wala hasione kuwa aibu ni kitu cha kujali? Maana alielewa vizuri sana kuwa, kile kinachomfanya mtu aone kuahibika, na hivyo kutovumulia anapodhulumiwa ni umwili, ambao umejengwa juu ya uongo kwamba unao heshima na mamlaka yake. Pia, alielewa vizuri kwamba yeye ni kiumbe kilichoko kiwandani, kinaofanywa upya (kwa kubomolewa zile tabia zilizojengeka kwa huo uongo), kwa kupewa ufahamu ulio sawa na ule wa yeye aliyeuumba huu mwili-Wakolo.3:10. Alielewa pia kwamba, katika huu mwili, tusipoumbwa Zaidi, hatuwezi kufanya chochote ili kujiendeleza, iwe ni kupata ufahamu, au uwezo wa kuutumia huo ufahamu kujenga tabia zetu, maana anakiri wazi kwamba, hawezi kufanya chochote kwa nguvu zake mwenyewe-Yohana.5:30.
Mwisho, alielewa pia anaowajibu, na uhuru wa kuamua kama, atamsikiliza na kumkubali Mungu kama asemavyo katika neno lake, au Shetani kama anavyoshawishi kupitia kwa, sheria iliyo katika tamaa za mwili na, iliyo pinzani ya ile ya Mungu, au la-Warumi.7:23. Kwa wale wote ambao tumeamua kumuiga kristo, ni lazima tuwe katika hii hatua ya uamuzi kati ya hizi sauti mbili, na utekelezaji wake, iwe ni, baraka au laana; baraka kwa wenye kuyafuata maagizo ya Mungu, na, laana kwa wenye kuyakataa( kwa kufuata ya Shetani)-Kumbukumbu.11:26. Ni wapi hapo haswa? Ikiwa kweli tumemwamini Mungu kama watu waliofundishwa, au wanaojifunza kwa kristo, basi, ufahamu tulionao, ambao ndio tunaounena katika maneno yetu, si wetu, mbali ni wa Mungu-Yohana.7:16.
Hii ni kwasababu, tuko kwenye hatua ya kuumbwa ufahamu wa Mungu( Mungu anaandika sheria zake mioyoni mwetu), na kuutumia kama nia za mioyo yetu ili kuumbika tabia yake-Waeb.8:10-11. Kwa sababu hii, woga wetu, huzuni, hofu, na kuona aibu kwetu, si kwa watu wala kwa maneno wanayotunenea, au kwa matendo wanayotutendea, mbali nikwa Mungu, na kwa neno lake- Isaya.8:12-13; Yerem.10:1-3; Mat.10:28. Kuwapi basi kuona aibu kwa sababu ya matamshi au dhuluma za wanadamu? Eeee, kuwapi kuwanung’unikia wanadamu wenzetu? Tunatafuta nini kwao?
MASOMO NA MITIHANI
Kulaumu au kunung’unikia wanadamu kwa mabaya wanaotutendea, au kulalamika kwa aina yeyote ya mateso au shida tunazozipata katika haya Maisha, ni kumkosoa Mungu, na ndio hapo anamshangaa yeyote anayejishirikisha katika hiyo akili, maana anamwambia huyo mtu; wewe unapindua mambo; je, mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichoumbwa kimwambie muumba kwamba hana akili-Isa.29:16? Eeee; tunanung’unika na kalaumu wengine, ilhali tunaelewa kabisa kwamba, hakuna yeyote awezaye kupinga chochote anachofanya Mungu-Isa.46:9-11. Kwa nini basi yeye aliye mwenye vyote na juu ya vyote awaache watu, au matatizo na shida zitukabe( ujumbe wetu, “mchakato wa uumbwaji wa mwanadamu”, unao maelezo Zaidi)? Ikiwa tumekubali kwamba bado hatujakamilika kuumbwa, kwamba haya Maisha ya mwili ni wakati wa kuumbika ufahamu na tabia za Mungu, basi tumekubali pia hatujui chochote isipokuwa kile Mungu anatufundisha. Yeye aliye mfano na mtangulizi wetu, ambaye ni kristo-Waeb.12:2, anayathibitisha haya akisema, mwana hatendi chochote kile, isipokuwa kile anaona baba akitenda-Yohana.5:19.
Kama ni hivyo basi, wakati tunalaumu mtu, au hali mbaya, huku tukiogopa na kuhuzunika, ni nani huwa ametufundisha kufikiria hivyo? Kristo tunayemuiga na kufuata nyayo zake anatuambia; yupo anishuhudiaye, nami najua ushuhuda wake( Mungu) ni kweli; tena, maneno ninayoyasema si yangu, niliambiwa na Mungu-Yohana.5:32; 7:16. Tunaelewa kabisa kwamba, ili mtu afikirie na kuongea jambo, ni lazima awe amelisikia kutoka mahali. Hapa Kristo ametuambia kuwa, asipojifunza kwa Mungu, yeye hajui,na wala, hasemi au kutenda chochote. Basi je, sisi tunaojisema kufuata nyayo zake, tunaponung’unika, kulalamika na kulaumu wengine kwa yale yanayotupata, je,tunafanya hivyo kwa sababu ni Mungu ametufundisha? Asha hata kidogo.
Maana haiwezekani Mungu akatuambia kwamba, mambo yote yatupatayo utendeka kwa wema wetu-Warum.8:28; na kwa hivyo, tuhesabu kuwa ni furaha tunapopatwa na haya mabaya-Yakubu.1:2, huku tukimshuru, kwa maana ni mapenzi yake kwetu sisi- 1 wathes.5:18, halafu arudi atuambie kwamba tuogope na kuhuzunika, huku tukilalamika na kuwalaumu wengine. Haiwezekani hata kidogo maana, Mungu habadiliki, wala hakosei eti, ahitaji marekebisho-Mal.3:6; Waeb.13:8.
Kwa hivyo, ni kweli kabisa kuwa, hizi dhuluma, matezo na shida katika haya Maisha ya sasa, ni sehemu za njia ya Mungu ya kutuumbia ufahamu na tabia. Akiyashuhudia hayo, huyu hapa anasema, kumbuka njia ninazokupitisha jangwani kwenye mateso, nikikujaribu, ili niyajue yaliyomo moyoni mwako, na kuthibitisha kama kweli umeamua kunitii au la-Kumbu kumbu.8:2. Ndugu na marafiki zangu, ikiwa tumekubali kwamba tuko kiwandani mwa Mungu ambapo anaendelea kutuumba, basi tukubali pia hatujui zile njia anazotumia kufanya hivyo, maana wakati alikuwa akipanga vile atatuumba, hatukuwepo. Itawezekanaje basi, tuanze kumshauri vile anapaswa kutuendesha, huku tukimwambia vile hali fulani ni mbaya au haifai? Ni nani huwa anatupa hayo mafikira ilhali, Mungu anasema mambo yote ni mazuri kwa uumbwaji wetu?
NI SHETANI
Nimesikia wengi wa wale ambao wamemwamini Mungu, na wanaojitahidi kufuata nyayo za kristo, wakishangaa na kuuliza ni kwa nini Mungu alimwacha Shetani aendelee kuwa hapa Duniani ilhali, anaelewa vizuri sana kuwa, nia yake ni kumwangamiza mwanadamu. Jibu la swali hili ndilo ule ufahamu utakaomwezesha yeyote aaminiye, kuishi bila kunung’unika wala kulaumu yeyote, na badala yake, kufurahi katika Bwana siku zote na katika kila hali-Wafilip.4:4, na kumshukuru kwa mambo yote-Waef.5:20. Tufananishe haya Maisha ya kimwili na nini? Yanafanana na mtoto ambaye amejiunga na shule ya msingi, kwenye darasa la kwanza ili aelimike. Huyu mtoto hajui kusoma au kuandika, na wala hajui herufi, au nambari yeyote.
Basi, kile anachosikia mwalimu akisema ndicho yeye ushika na kuanzia hapo, yeye ukifahamu hivyo alivyofundishwa. Baada ya wakati fulani, mwalimu anampa huyo mtoto mtihani, akitaka kuthibitisha kama kweli alishika kile alimfundisha. Basi, hapo mwalimu anapouliza swali kuhusiana na alichomfundisha, yeye utoa aina kama nne za majibu, na kumwagiza mtoto achague mojawapo ambalo ndilo sahii( ya kweli). Kwa vile huyo mtoto hajui kinginecho isipokuwa kile alifundishwa na mwalimu, yeye bila kuharibu wakati, uchagua lile jibu sahii, maana tayari alishafundishwa hivyo, na hapo yeye uhesabiwa kuwa amehitimu, au kufaulu.
Wapenzi, tuko hapa katika haya Maisha ya kimwili kwa kusudi la Mungu, la kuendelea kutuumba. Na ile njia analotumia kutuumba ndilo anatufundisha katika neno lake; kumaanisha kwamba, nje ya hilo neno, hatujui chochote, na hivyo hatuwezi chochote, maana, roho yake ndiyo inatuumba katika huu mwili, na pumzi yake inatupa uhai-Ayub.33:4. Hii roho ya Mungu pia, ndio mkono wake, maana anazidi kutuambia kwamba, mikono yake ilitufanya, ikatutengeneza-Zab.119:73.
Ninalolisema ni hili, tumeumbwa, na tunaendelea kuumbwa, kufanywa viumbe wa kiroho, katika roho ambayo ndilo hili neno tunalofundishwa-Wakol. 1:16; Yohana.6:63; maana kristo mwenyewe ambaye ndiye mfano wetu, eee, ndiye kile tutafanyika tukikamilika, anaitwa neno la Mungu-Ufu.19:13 ( kwa maelezo Zaidi, soma ujumbe uitwao, “wewe ni nini?”). Basi, Baada ya kuwa Mungu ametufundisha haya Maisha yake, kama mwalimu anayetaka kuhakikisha wanafunzi wake wameelewa na kuelimika vilivyo, yeye utuwekea mtihani. Mfano: Yeye ametuambia Maisha yake ( ambayo ndilo hili neno analoliumba ndani yetu ili iwe, ufahamu tunaotumia kuishi), ni upendo usio na masharti- Warumi.13:10; 2yohana.1:6; 1 Wakor.13:4-8.
Hali tukielewa hayo, jirani zetu wanatujia kwa matusi na madharau, au wanatunyang’anya mali zetu. Na papo hapo, Mungu anatuuliza; mnapaswa kuwafanyia nini watu wa aina hii? Wazo linatujia kuwa, hawa ni watu wabaya sana. Tunajiuliza ni kwa nini wanatudhulumu? Akili inatuambia vile tunafaa, kuwakasirikia na kuwaonyesha uchungu tulionao, kwa kutokuwaongelesha. Saa yiyo hiyo, kumbukumbu linatujia, ya yale Mungu ametufundisha likisema; mpende adui yako; mtendee mema yeye akudhulumuye-Mat.5:44; Warum.12:14,17,20. Bila shaka, ikiwa tunafundishwa na Mungu, tutahusiana na hawa kulingana na anavyosema katika neno lake.
Anayetujia na haya mawazo, na mawaidha yaliyo kinyume na yale Mungu ametufundisha ni Shetani, na ni Mungu anamruhusu ili awe mtahini( anayetuwekea mtihani) wetu, maana anasema kumhusu huyu Shetani (ambaye, ndiye amewafundisha hawa wanaotudhulumu na kututendea mabaya); mimi nimemwacha huyu Shetani kupitia kwa maajenti wake- 2 wakor.11:14-15, ili niwajaribu( niwafanyie mtihani), na kuona kama mtatembea kama nilivyowafundisha au la-waamuzi.2:21-22.
NI ASHINDAYE
Shetani anaelewa vizuri sana kuwa Mungu anatuumba ili atupa utawala wa dunia hii tukiisha kamilika kuwa viumbe wa kiroho. Sasa hivi, Shetani ndiye mungu na mtawala wake. Anaelewa vizuri sana kwamba, tusipoumbika kuwa viumbe wa kiroho, (ambao itawezekana tu kwa wale watakaoumbika hili neno liwe Maisha yao ) tutakufa. Mungu katika kristo ametufundisha haya yote na kutuonya dhidi yake, akisema, jihadharini, maana mshitaki wenu shetani, anatafuta kuwadanganya awatoe katika uhai ili mfe.
Hali mkikumbuka yale niliyowafundisha, mpingeni-1 petro.5:8. Na kuhusiana na hawa watu ambao tayari amewadanganya na kuanza kuwatumia kama maajenti wake-2 wakor.11:14, na ambao ndio hawa wanaotudhulumu, Mungu ameshaa tuonya dhidi yao akisema, tazameni nawatuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Mwe werefu kama nyoka, na wapole kama jiwa-Mat.10:16. Msipigane au kushindana na wao, mbali mwaepuke-2Tim.3:5. Itawezekanaje na kuaje, mtu atutukane, kututapeli, atufanyie madharau ya kila aina, halafu tusimfanyie chochote ? Kristo, ambaye ndie kielelezo na mfano wetu, hakupigana au kushinda nao kwa chochote kile. Aliyafumilia mapingamizi makuu kutoka kwa watendao uasi-Waeb.12:3; yeye hakutenda dhambi wala hila haikuonekana kinywani mwake. Alipotukanwa, hakurudisha matukano-1 Petro.2:21-22. Kwa nini tujiachilie hivyo?
MAISHA MAWILI TOFAUTI
Maisha ya ulimwengu huu wa sasa yamejengwa juu ya msingi wa kiburi-1 Yohana.2:16, ambacho kinaingia kwa kila mtu aaminiye uongo wa kwamba, yeye ni kama Mungu-Mwa.3:5. Basi, kila mtu anajisimamia kwa kila afanyacho, huku akitaka wenzake wamkubali kama mtu aliye mkuu. Ijapokuwa wako na Mungu kwa midomo yao, hawamtambui wala kumtegemea kwa chochote kile wafanyacho. Na kwa vile wanaamini uongo, basi yote watendayo ni ya kuharibu. Mungu naye amewaacha wafuate akili zao zizizofaa-warum.1:28-31. Kwa vile wao ni nyumba ambazo ujenzi wake haujakamilika bado, huku wakijaribu kujijenga, jambo ambalo haliwezekani-Zab.127:1; Yohana.15:5, Walichofaulu kufanya ni kuichafua dunia, na kujiharibu wenyewe- Isa.24:5-6.
Kristo alikuja kufumbua macho ya wanadamu, wapate kujielewa na kuwacha huu uongo-Isa.42:6-7. Katika ufunuo wake, ametufundisha kwamba, sisi katika huu mwili , ni mjengo ambao mjenzi wake wa pekee ni Mungu, na asipotujengaZaidi, jitihada letu la kujiendeleza litabomoa hicho alichokijenga na tutajiharibu-yohana.5:30; Mwa.2:17. Na kama vile mjengo hauongeleshi mjenzi kumshauri namna ya kuujenga, na vivyo hivyo, sisi hatuwezi kumshauri Mungu vile ataendelea kutuumba, au, vile vifaa atakavyotumia-Isa.55:7-9. Basi, kama vile tulivyoona awali, Shetani na wale amedanganya ambao wao ni miungu ya uongo, wanatumika na Mungu, kama njia ya kuthibitisha msimamo wa uamuzi wetu-Yakubu.1:2; Kumbukumbu.8:2-3. Kwa vile sisi hatujiiti kitu isipokuwa kile neno la Mungu linatuambia, basi, wanapokuja na matendo yao ya uovu, kwetu yanakuwa ni furaha.
Ni ngazi ya kutushikanisha na Mungu Zaidi, na wala sio kikwazo, maana hapa ndipo tunakumbuka kutenda vile Mungu ametufundisha, huku tukikataa yale wanatushawishi kwayo( soma ujumbe uitwao, “ wewe ni nini?”, kwa maelezo ya ndani)-Mat.4:4, 7, 9,11. Hii ndio sababu, tunafurahi wakati maudhi yanatupata, maana kupitia kwa hayo, tunaumbika tabia, wakati tunaendelea kutenda ya Mungu na kupinga ya Shetani-warum.5:3-4.Na kwa vile tunajua kwamba, kile wanajiita ni uongo, na pia kwamba, hawajui chochote kuhusu Maisha-Yerem.8:9; warum.1:22, basi, wanapotusifu au kutudharau, ama kutudhulumu, hatuyatilii maanani, kwasababu tunaelewa kwamba, hawajui wasemalo wala watendalo-Matendo.7:60;Luka.23:34.
Pia, tunaelewa kwamba, Mungu amewaachilia ili kuthibitisha uamuzi wetu hapo tunapokataa ushawishi wao, na kupinga moyo wa kimwili ambao kila wakati, unatamani kujikweza kama wao-Wagal.5:17. Ndugu zangu, je,hapa kunao nafasi au sababu ya kunung’unika, kulalamika, wala kulaumu? Hawa ni watu ambao hatuendi njia moja na wao, wala hatuhusiani kwa jambo lolote.
Tunaanzana wapi na wao hata tunung’unike na kulalamika kwa matamshi au matendo yao? Mungu anasema vizuri sana kwamba, kwetu sisi hawapo, nasi kwao, hatupo-Wagal.6:14. Wapenzi, Katika Maisha ya uungu aliyoyafundisha kristo, hakuna woga, huzuni, hofu, kulaumu, kulalamika, au kunung’unika, mbali, kunao kufurahia na kushukuru kwa kila jambo, na katika kila hali, maana ni njia ya Mungu ya kutuumba tabia ya utakatifu hata tuufikie ukamilifu-1 Wathes.5:18; Waef.5:20. Kila mtu hapa amebaki na uamuzi wa kufanya. Utakubali wewe ni kile Mungu amekuambia, na kujiweka mikononi mwake ili aendelee na kazi yake ya kukukamilisha au, utaendelea na uongo wa Edeni wa kujigamba na kutetea uongo?
Ni mwokozi wetu, aliye pia kuhani na Bwana wetu, Kristo, akiendelea kutufundisha ili,tuweze kuifikia kusudi la Mungu la kutuumba, yaani, uzima wa milele-1Yohana.2:25. Yote ameyalete kwako kupitia kwa mtumishi wake.
ENDTIME CHURCH OF GOD: WEBSITE >www.endtimecog.org